Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 120 wamekufa kutoka na mafuriko na maporomoko ya udongo Kenya:OCHA

Nairobi Kenya
Ouri Pota
Nairobi Kenya

Watu 120 wamekufa kutoka na mafuriko na maporomoko ya udongo Kenya:OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Mafuriko makubwa na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Kenya yamasebabisha vifo vya watu 120 na uharibifu mkubwa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva hii leo msemaji wa shirika hilo Jens Laerke amesema mvua zaidi zinatarajiwa kunyesha katika wiki zijazo na kwamba hadi sasa,“watu zaidi ya 160,000 wameathirika na katika kisa kimoja cha Novemba 22, watu 72 walipoteza maisha baada ya maporomoko ya udongo kuzika nyumba zao kwenye Kauti ya Pokot Magharibi, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyi.”

Ameongeza kuwa tahadhari ya mafuriko imetolewa katika majimbo ya Pwani, Kaskazini na Magharibi mwa nchi huku kukiwa na hatari kubwa ya maporomoko ya udongo na matope katika sehemu za katikati na bonde la ufa.

OCHA imesema ili kusaidia juhudi za misaada ya dharura za serikali na shirika la msalaba mwekundu la Kenya na wadau wengine, inakusanya mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu kusaidia kuratibu misaada hasa katika maeneo ambako madaraja na barabara zimeharibiwa na mafuriko.

Mashirika ya misaada hadi sasa yamefikisha misaada ya chakula na vifaa visivyo chakula, timu za dharura za wahudumu wa afya, maji katika jamii zilizoathirika zaidi na kufanya tathimini kwa njia ya anga kubaini jamii zisizofikika.  OCHA inasema “inakadiriwa kwamba fedha za ufadhili zinazohitajika kwa kukabiliana na janga hili n idola milioni 15 ili kuruhusu mashirika ya kibinadamu kutoa msaada muhimu wa chakula na kujikimu kimaisha , maji, usafi, malazi na huduma za afya kwa watu katika maeneo yaliyoathirika zaidi.”

Shirika hilo limesema janga la mabadiliko ya tabianchi kwa hakika linaongeza mahitaji ya kibinadamu nchiniKenya nae neo zima la Afrika Mashariki. Janga la mabadiliko ya tabianchi linavyoongezeka Maisha ya watu yanasambaratishwa na fursa zao za kupata mahitaji ya msingi kama chakula na maji safi na salama zinazidi kuwa finyu.

Katika misimu mitatu ya mvua iliyopita kwenye Pembe ya Afrika kumeshuhudiwa ukame mara mbili na sasa mafuriko makubwa. Kenya tayari ilikuwa inakabiliwa na njaa kabla ya mafuriko, huku watu milioni 3.1 wakitarajiwa kuwa katika mgogoro na dharura ya kutokuwa na uhakika wa chakula tangu Oktoba mwaka huu.