Watoa huduma 4 wa Ebola wauawa DRC

28 Novemba 2019

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wahudumu 4 wa Ebola wameuawa kufuatia shambulio la usiku wa kuamkia leo  huku wengine 5 wakijeruhiwa.
 

Shirika la afya duniani, WHO limesema shambulio hilo limetokea katika kambi ya Biakato ambako pia kuna ofisi ya WHO ya uratibu wa masuala ya Ebola.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt.Tedros Gebreyesus amesema kuwa shirika lake wamevunjika moyo kutokana na kitendo hicho akisema kuwa, “hofu yetu kubwa imekuwa ni kushambuliwa na leo yametimia. Msimamo wetu sasa ni kutunza majeruhi na kuhakikisha kuwa watumishi wengine wako salama.”
Akipatia msisitizo kauli hiyo, Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika Dkt,  Matshidiso Moeti, ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa huku akitakia ahueni mejeruhi.
Kwa mujibu wa WHO, waathirika wa tukio hilo ni mfanyakazi wa timu ya utoaji chanjo, madereva wawili na afisa wa polisi. 
Shirika hilo limesema hakuna mtendaji wake aliyeuawa lakini wamehuzunishwa sana.
 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter