Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuko tayari kuimarisha usalama kwenye harakati dhidi ya Ebola- MONUSCO

Walinda amani wa MONUSCO wasema wako tayari kuimarisha usalama kwenye harakati za kukabiliana na Ebola.
MONUSCO
Walinda amani wa MONUSCO wasema wako tayari kuimarisha usalama kwenye harakati za kukabiliana na Ebola.

Tuko tayari kuimarisha usalama kwenye harakati dhidi ya Ebola- MONUSCO

Amani na Usalama

Wakati suala la ukosefu wa usalama likitajwa kuwa ni moja ya changamoto katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola huko jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO umesema unasubiri kutambua ni jinsi gani itatoa usaidizi wake.

Radio Okapi iliyo chini ya MONUSCO imesema tayari Naibu Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC David Gressly ametembelea Beni, ambako amepongeza serikali ya nchi hiyo kwa hatua za haraka ilizochukua kutangaza kuwepo kwa ugonjwa huo.

“Tutatembelea Mangina. Yote hii inadhirisha kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa. MONUSCO itashiriki kwenye hatua za kukabiliana an Ebola na tutachangia msaada wa vifaa. Iwapo kuna suala la usaidizi kwenye usalama, tuko tayari kufanya hivyo,” amesema Bwana Gressly akiwa mjini Beni.

Mangina, mji ulioko eneo la Beni jimbo la Kivu Kaskazini, ndio eneo ambako kumeripotiwa visa vya Ebola, katika mlipuko huu wa 10 wa ugonjwa huo nchini DRC.

Serikali ya DRC ilitangaza juzi mlipuko wa Ebola jimboni Kivu Kaskazini, ikiwa ni siku chache tu baada ya mlipuko huo kutangazwa kumalizika huko jimboni Equateur.