Kituo cha kutibu Ebola Butembo chashambuliwa, UNICEF yafunguka

“Nachukizwa na shambulio la hivi karibuni zaidi dhidi ya kituo cha kutibu Ebola huko Butembo, jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC,” ndivyo ilivyoanza taarifa iliyotolewa jioni ya leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, mjini New York, Marekani.
Taarifa hiyo inazungumzia shambulio la Jumatano kwenye kituo hicho kinachoendeshwa na madaktari wasio na mipaka, MSF ambapo afisa mmoja wa polisi aliuawa na kituo kuchomwa moto.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore ametuma salamu za rambirambi kwa familia na ndugu wa mtumishi huyo pamoja na MSF akisema kituo hicho kinahudumia watoto na familia zao.
Hili ni tukio la pili ndani ya wiki moja ambapo Bi. Fore amepongeza shirika la afya ulimwenguni, WHO, MSF na ALIMA na mashirika mengine kwa kuendelea kuhudumia wananchi katika mazingira magumu.
“Kila siku, wafanyakazi wa UNICEF na wadau wetu wakiwemo wahudumu wa afya kwenye vituo vya matibabu na jamii wanafanya juhudi za kishujaa kuokoa maisha ya watoto na watu wazima ambao wameathiriwa na Ebola,” amesema Bi. Fore.
Amesema kazi hiyo inafanyika dhidi ya kikwazo kikubwa ambacho ni mlipuko wa pili kwa ukubwa kwenye historia ya Jamhuri ya Kidemorkasia ya Congo, DRC na kwamba ni jambo la kusikitisha kuwa kuna watu ambao wanaska kupora watoto haki yao ya msingi ya kuishi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNICEF amesema njia pekee ya kutokomeza Ebola ni kwa wahudumu wa afya, UNICEF, wadau kuweza kufanya kazi kwa usalama kwenye jamii zilizokumbwa na ugonjwa huo, ikiwemo maeneo ya ndani zaidi.
Amesisitiza kuwa vituo vya afya katu havipaswi kuwekwa rehani kwa kukosesha usalama mashariki mwa DRC.
Zaidi ya watu 800 nchini DRC wameathirika na Ebola katika mlipuko huu hivi kairbuni zaidi ulioanza mwezi Agosti mwaka jana ambapo 500 kati yao wamefariki dunia.
Hata hivyo kwenye maeneo kama Mangina, Beni, Komanda ugonjwa umedhibtiwa kwa kiasi kikubwa ambapo zaidi ya watu 250 wamepona na 80,0000 wamepatiwa chanjo dhidi ya Ebola.