Baraza la Usalama lapitisha azimio kuchagiza harakati dhidi ya Ebola DRC

30 Oktoba 2018

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa wajumbe wa Baraza la Usalama kwa kauli moja wamepitisha azimio ambalo pamoja na kuchagiza harakati za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC , limelaani vikali mashambulizi na mauaji  ya watoa huduma za afya ambao wanaweka rehani maisha yao kutokomeza ugonjwa huo hatari.

WHO/Lindsay Mackenzie
Timu ya kutoa chanjo dhidi ya Ebola iliyopiga kambi huko kijiji cha Iboko, wakiwa na pipa lenye chanjo wakielekea eneo la Bisolo. Hii ni tarehe 20 juni 2018

Azimio hilo lililoandaliwa na Ethiopia na Sweden limepitishwa wakati wa kikao kuhusu amani na usalama barani Afrika kikijikita jinsi Ebola inavyotishia usalama nchini DRC na nchi jirani.

Wajumbe wote 15 wa Baraza la Usalama waliridhia azimio hilo namba 2439 la mwaka 2018 ambapo punde baada ya kupitishwa, mwakilishi wa kudumu wa Ethiopia kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Taye Atske Selassie Amde pamoja na kushukuru wajumbe wote wa kuridhia azimio hilo amesema, « Tunatumai kuwa azimio tulilopitisha leo litatuma ujumbe thabiti na pia kuchangia katika kuhamasisha usaidizi wa kimataifa katika kudhibiti mlipuko wa Ebola. »

 Awali akizungumza na waandishi wa habari kufafanua kuhusu azimio hilo mwakilishi wa kudumu wa Sweden kwenye Umoja wa Mataifa Balozi  Olof Skoog amesema azimio linatuma ujumbe, "Mosi ni  ujumbe wa kuunga mkono siyo tu wa wale walio mstari wa mbele kukabili janga hili, bali pia kazi inayofanywa na WHO, MONUSCO na bila kusahau serikali ambayo iko katika harakati za udhibiti. Ni wazi kuwa juhudi zaidi zinahitajika na hivyo azimio linataka jamii ya kimataifa ishiriki zaidi kutoa mchango wa fedha na  kwa mantiki hiyo Sweden ambayo tayari inatoa msaada, inafikiria kuongeza zaidi msaada huo na tunasihi wengine pia wafanye hivyo."

Amesema ujumbe wa pili ni ule wa kulaani mashambulizo yote yanayofanywa na vikundi vilivyojihami dhidi ya raia na watoa huduma ya afya, akiongeza kuwa , "hebu na niweka wazi kuwa wanawake na wanaume walio mstari wa mbele kukabili ugonjwa huu wakiweka hatarini maisha  yao ili kuokoa maisha ya wengine, wana haki ya kupata heshima na ulinzi kutoka kwetu.  Katu hawapaswi kuwa walengwa iwe DRC au kwingine."

Balozi Skoog amesema misingi ya kibinadamu lazima izingatiwe popote na wakati wowote na azimio la leo linazingatia hilo katika kukabili Ebola DRC.

Baraza la Usalama la Umoja waMataifa limekuwa likifuatilia kile kinachoendelea huko DRC kuhusiana na Ebola ambapo tarehe 28 mwezi Agosti mwaka huu, kufuatia ombi la Sweden, wajumbe walipatiwa taarifa ya hali halisi na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. Tarehe 3 mwezi huu wa Oktoba wajumbe walipatiwa tena muhtasari wa hali halisi kuhusu Ebola na mkuu huyo wa WHO ambapo aliwaeleza kuwa "harakati za vikundi vilivyojihami huko jimboni Kivu Kaskazini hususan eneo la Beni zinakwamisha juhudi za WHO za kudhibiti Ebola na wakati mwingine inabidi zisitishwe."

Dkt. Ghebreyesus aliomba wajumbe wa Baraza walichukua hatua za dhati kudhibiti hali hiyo ya ukosefu wa usalama.

Ugonjwa wa Ebola ulibuka Kivu Kaskazini na Ituri mwezi Agosti mwaka huu. Hadi tarehe 23 mwezi huu wa Oktoba, WHO imeripoti visa 212 vimethibitishwa na visa 35 ni shukiwa.

Halikadhalika kuna watu 159 walioripotiwa kufariki dunia kutokana na Ebola ambapo huu ni mlipuko wa pili wa Ebola nchini DRC kwa mwaka huu.

Mlipuko wa awali  huko jimbo la Equateur ulisababisha vifo 54 na ulitangazwa kuwa umetokomezwa tarehe 24 Julai mwaka 2018.

Hata hivyo kamati ya dharura ya WHO iliamua kuwa kulingana na hali ya sasa, bado hakuna hakikisho la kutangaza kuwa Ebola ni dharura ya kimataifa. 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud