Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya WMO yabaini ongezeko la hewa chafuzi katika anga

Wingu katika eneo la Plechotice, Slovakia
WMO/Monika Nováková
Wingu katika eneo la Plechotice, Slovakia

Ripoti ya WMO yabaini ongezeko la hewa chafuzi katika anga

Tabianchi na mazingira

Ripoti ya shirika la hali ya hewa duniani WMO iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi imeonesha ongezeko zaidi la hewa chafuzi katika anga. Hali hii inayoendelea kwa muda mrefu  inaamaanisha kuwa vizazi vijavyo vitakabiliana na ongezeko la matokeo mabaya ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la joto, mabadiliko makubwa ya hali uya hewa, upungufu wa maji, kuongezeka kwa kina cha bahari na uharibifu kwa viumbe wa majini na ardhini.

Chapisho la WMO kuhusu hewa chafuzi limeonesha kuwa viwango vya wastani vya hewa ya ukaa (CO2) viliongezeka na kufikia kufikia 407.8 kwa milioni moja mwaka 2018 ikilinganishwa na kutoka 405.5 kwa milioni mwaka 2017.

Ongezeko la hewa ukaa yaani CO2 kutoka mwaka 2017 hadi 2018 lilikuwa karibu sawa na lile lililoshuhudiwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2017 na juu kiasi ya wastani kwa muongo mmoja uliopita. Viwango vya kimataifa vya CO2 vilipita kiwango cha juu cha 400 kwa milioni katika mwaka 2015.

Wataalamu wanasema kuwa hewa ukaa inasalia katika anga kwa karne kadhaa n ahata zaidi inapokuwa baharini.

Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas anasema, “hakuna dalili ya kupungua kwa mkusanyiko wa hewa chafuzi katika anga licha ya ahadi zote za mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Tunahitaji kutafsiri ahadi hizo kwa vitendo na kuongeza kiwango cha matamanio kwa ajili ya ustawi wa baadaye wa jamii.”