Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimesikitishwa na matokeo ya COP25 lakini sitakata tamaa- Katibu Mkuu wa UN

Maandamano ya vijana katika mkutano wa COP25
UNFCCC
Maandamano ya vijana katika mkutano wa COP25

Nimesikitishwa na matokeo ya COP25 lakini sitakata tamaa- Katibu Mkuu wa UN

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo, amesema amesikitishwa na matokeo ya mkutano wa mabadiliko ya tabiachi ambao umekamilika leo mjini Madrid, Hispania.

Kwa mujibu wa Bwana Guterres, washiriki wa mkutano huo wameipoteza fursa ya kuchukua hatua muhimu ya kukabiliana na janga la tabianchi lakini hatakata tamaa na hivyo akaisihi jumuiya ya kimataifa kutokata tamaa pia.

“Jumuiya ya kimataifa imepoteza fursa muhimu ya kuonesha utayari ulio thabiti zaidi wa kuchukua hatua za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kukabiliana na athari zake na kuzifadhili nchi zinazoendelea.” Amesema Guterres.

Ilikuwa imetegemewa kuwa nchi zitaweka ahadi zaidi, kwanza, kupunguza hewa chafuzi kwa kiwango ambacho kingeweza kutimiza lengo la Mkataba wa Paris wa kuhakikisha ongezeko la wastani la joto duniani halivuki nyuzi joto 1.5, lakini hilo halikutokea.

Katibu Mkuu Guterres akiisihi jumuiya ya kimataifa amesisitiza, “hatutakiwi kukata tamaa, na sitarudi nyuma. Zaidi kuliko wakati mwingine wowote, nimejizatiti kuhakikisha kuwa katika mwaka 2020 nchi zote zinaweka ahadi ya kuchukua hatua ambazo wanasayansi wanatumbia ni muhimu ili kufikia “usawa wa hewa ya ukaa” kufikia mwaka 2050 na kuzuia joto kuongezeka zaidi ya nyuzi joto 1.5.”

Tweet URL

 

Ili kufikia hatua hiyo, inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2030 ni muhimu kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi kwa asilimia 45, na kufikia katikati mwa karne hii, kuhakikisha uzalishaji wa hewa ukaa hauzidi kiwango cha hewa chafuzi ya CO2 ambayo asili ya dunia inaweza kuchukua. Kwa sasa, viwango vinaendelea kuongezeka na kwa mujibu wa utabiri, viwango vinaweza kuongezeka kwa nyuzi 3-4 na hii inaweza kumaanisha kwamba sayari haitafaa kwa maisha ya binadamu.

Pamoja na kwamba majadiliano yamedumu kwa takribani siku mbili zaidi ya muda wa wiki mbili uliokuwa umepangwa, pamoja na mivutano ya usiku na mchana, washiriki hatimaye wameipitisha nyaraka ambayo haina hatua maalum na majukumu ya nani atafanya nini.