Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sijawahi kushuhudia amani maishani mwangu: Mkimbizi Rotto

Maelfu ya wakimbizi wa ndani wakiwa wamekusanyika katika eneo la kanisa la Emmanuel huko Yei, Sudan Kusini.
UNHCR/Rocco Nuri
Maelfu ya wakimbizi wa ndani wakiwa wamekusanyika katika eneo la kanisa la Emmanuel huko Yei, Sudan Kusini.

Sijawahi kushuhudia amani maishani mwangu: Mkimbizi Rotto

Amani na Usalama

Tangu nizaliwe sijawahi kushuhudia amani, hiyo ni kauli ya mkimbizi wa ndani wa Sudan Kusini John Rotto mwenye miaka 65, aliyezaliwa na kukulia kwenye vita.kulikoni? 

Katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Rimenze ndio maskani ya Rotto ambaye anatumai hataaga dunia akiishuhudia nchi yake bado iko vitani. Wakazi wa eneo hiliwalidhani kuna matumaini taifa lao lilipopata uhuru 2011,  Rotto akadhani ni wakati wa kupumzika na kupunga upepo ili kujenga upya maisha na mustakabali bora. 

Lakini miaka miwili tu baada ya uhuru huo zahma ikazuka upya ikiwemo kijijini kwake Equatoria Magharibi ambako maelfu ya watu walikabiliwa na ukatili mkubwaikiwemo wa kingono na kuwalazimisha kufungasha virago “Nyumba yangu ilichomwa moto mara mbili, mwaka wa kwanza nilikimbilia katika kambi hii na nikaikarabati utulivu uliporejea, kisha ikateketezwa tena, haya ndio madhila ninayoyapitia

Kwa kuwa sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi na familia yake Rotto hawezi tena kupata kipato kutokana na kilimo na badala yake anategemea utengenezaji wanyavu za kuvulia samaki ili kuishi, na kipato apatacho kwa siku ni takribani dola tatu na nusu “Hii ndio kazi ninayofanya ili kuweza kuishi kwa sababu haturuhusiwi kwenda nje ya kambi kulima”

Baada ya kuanzishwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa hivi karibuni Rotto na wenziwe wanaitaka amani kwa udi na uvumba "Bado tuna hofu, hatujaihisi amani ingawa tunaisikia, tunapaswa kuihisi huduma ya amani hii na ndipo itakuwa amani ya kweli.”

Watoto wa Rotto pia wamezaliwa vitani na anahofia mustakbali wao wasijepitia alichopitia

“Hakuna amani, watoto wangu wawili wamezaliwa vitani.Sijui jinsi gani serikali itawasaidia watoto hawa kukua bila milio ya risasi. Vita vimeathiri akilizao na wamekuwa kama wendawazimu.”

Japo amekatishwa tamaa mara nyingi na miakataba ya amani inayovunjika safari hii anatumai kwamba fikra zake si sahihi na kwamba viongozi watawapa watoto wakeusalama na mustakabali bora wanaostahili.