UNMISS imelaani vikali mashambulizi mapya kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Adidiang Upper Nile
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS, umelaani mashambulizi mapya na ghasia zinazofanywa na watu wenye silaha, zinazolenga wakimbizi wa ndani wanaotafuta hifadhi katika eneo la kisiwa cha Adidiang, kilichoko takriban kilomita 40 kusini mwa mji mkuu wa jimbo la Upper Nile wa Malakal.
Kwa mujibu wa taarifa ya UNMIS iliyotolewa leo baadhi ya taarifa za waathirika zinaonyesha kuwa idadi kadhaa ya raia waliokimbia wanaweza kuwa walikufa maji katika Mto Nile.
Takriban raia 5,000 walikimbilia eneo hilo mwezi uliopita, kufuatia mapigano makali kati ya makundi hasimu yenye silaha huko Tonga, magharibi zaidi yam ji wa Malakal.
Shambulio la hivi punde pia limezua mapigano makali kati ya makundi na jamii tofauti za wakimbizi wa ndani katika eneo la ulinzi wa raia la UNMISS (POC) ambapo wafanyakazi wa UNMISS walijibu haraka kurejesha utulivu na kutoa ulinzi thabiti kwenye eneo hilo.
UNMISS inatoa wito kwa washambuliaji kusitisha mapigano mara moja na kujiepusha kuwadhuru raia walio hatarini na wakimbizi wa ndani.
Ujumbe huo pia unatoa wito kwa mamlaka za serikali na kitaifa kuingilia kati haraka ili kupunguza hali hiyo na kulinda maisha ya raia.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wametumwa kwendfa kuokoa raia wanaozama majini na kutoa ulinzi kwa watu walioathirika.
UNMISS inawashirikisha wadau wote wanaohusika, ikiwa ni pamoja pande zinzokinzana, mamlaka, na jumuiya za mitaa ili kuwezesha kuchukuliwa hatua za pamoja kwa wakati muafaka.