Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante Zambia kwa kukirimu wakimbizi- Grandi

Kamishna mkuu wa UNHCR Fillipo Grandi akizungumza na vyombo vya habari. (Picha kutoka maktaba)
Credit English (NAMS)
Kamishna mkuu wa UNHCR Fillipo Grandi akizungumza na vyombo vya habari. (Picha kutoka maktaba)

Asante Zambia kwa kukirimu wakimbizi- Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Fillipo Grandi ameshukuru Zambia kwa ukarimu wake na kufungua milango kwa ajili ya wakimbizi huku akitoa wito kwa usaidizi zaidi kwa wenyeji wanaohifadhi wakimbizi. 

Ni katika soko lililopo eneo la makazi  ya wakimbizi la Mantalapa nchini Zambia, shughuli za biashara zikiendelea na punde ni ugeni, Kamishna Mkuu wa UNHCR Fillipo Grandi na  ugeni wake.. kisha akazungumza na wachuuzi, ambao ni mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, akiwauliza wateja wao ni akina nani..?

Mukea Chungu, mkimbizi kutoka DRC anasema,“katika soko hili, tunafanya biashara vizuri na tunashirikiana vyema na wazambia. Wakongo na wazambie ni wamoja na pia wametupokea vizuri na hata katika soko hili kuna wazambia wengi.”

Bwana Grandi akasema ni lazima kukumbuka kuwa wakimbizi wanapoingia, wanaoathirika mwanzoni kabisa ni jamii za wenyeji kwa kuwa ni lazima wagawane rasilimali chache zilizopo.

Kisha Bwana Grandi akatembelea mgahawa na kusalimiana na mmiliki wa mgahawa ambaye ni mzambia. Mmiliki huyo Jane Kabwe anasema ameajiri wakimbizi wawili na kwamba, “kama hawa wakimbizi hawangalikuwapo hapa, nisingalianzisha huu mgahawa kwa sababu nisingalikuwa na wateja.”

Kwa mujibu wa Grandi, UNHCR itaendelea kuwekeza kwenye hatua za dharura na pia za muda mrefu kwa ajili ya wakimbizi na wenyeji. Hata hivyo,“jambo muhimu zaidi ni kushughulikia sababu zinazosukumu watu kukimbia makwao na katika hili sababu kuu ni vita. Kwa  hiyo tunahitaji kuisihi jamii ya kimataifa ijikitie kwenye amani DRC na mchakato wa kisiasa unaoruhusu kumaliza kwa mvutano unaofurusha watu wake.”

Kwa mujibu wa UNHCR, Zambia inahifadhi zaidi ya wakimbizi 84,000 wengi wao wakitoka DRC, Somalia, Rwanda na Burundi.