Mipango ya kuwaokoa wahamiaji kutoka bahari ya Mediteraani haitoshi: UNHCR

Shirika la kuwahudumia wakimbizi la UNHCR , linasema linakaribisha hatua za mataifa kadhaa ya Ulaya za kumaliza mgogoro wa wahamiaji 450 waliokuwa wamekwama katika baharí ya Mediterrania kutokana na kutokubaliwa na taifa lolote kuingia nchini mwao.
Tangu Jumamosi, serikali za Ufaransa,Ujerumani, Italia, Malta, Hispania na Ureno ziliafikiana kutia nanga kwa meli hiyo nchi kavu na kwa pamoja kuwasaidia wahamiaji hao 450, na pia kushughulikia maombi ya hifadhi endapo yatatokea.
Hii leo mjini Geneva Uswisi, Kamishna mkuu wa wakimbizi Fillipo Grandi amesema, “tunatumai kwamba mpango huu sasa utatekelezwa kwa uhakika na haraka pamoja na kuwaondolea jinamizi watu hawa , na huu ni mfano mzuri wa jinsi gani kushirikiana kwa pamoja , nchi zinaweza kufanya uokozi na kulinda mipaka yake huku zikitimiza wajibu wa kimataifa kuhusu wahamiaji.”
Hata hivyo, Kamishna Grandi amesema ufumbuzi huu unapaswa kwenda mbali zaidi ya kushughulikia meli na kisa kimoja kimoja.
Ameongeza kuwa mipango ya sasa ya kushughulikia suala la wahamiaji barani Ulaya haitoshi na inapaswa kuwa ni ya suluhu ya muda mrefu yenye tija, usimamizi na mipango endelevu, la sivyo kuwasili kwa wahamiaji kutaendelea kuwa na suluhu ya muda mfupi na isioendelevu.
Wakati huohuo amesema wakati mataifa yana wajibu wa kuokoa maisha na kuwalinda wakimbizi, watu wanaookolewa hawana haki ya moja kwa moja ya kuchagua wapi wanakotaka kwenda. Wanatakiwa kutia nanga mahali ambapo pana usalama , ikiwa ni pamoja na wale watakaohitaji ulinzi wa kimataifa , lakini sio lazima ikiwa ni mahali wanapopondelea.