Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahueni kwa wahamiaji baada ya mkwamo Diciotti kumalizika

Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea

Ahueni kwa wahamiaji baada ya mkwamo Diciotti kumalizika

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeeleza furaha yake baada ya kumalizika kwa mkwamo wa wahamiaji 140 waliokuwa wamesalia kwa siku sita ndani ya meli ya uokozi ya Diciotti katika pwani ya Sicily nchini Italia.

Wahamiaji hao waliookolewa baharini Mediteranea, walikuwemo ndani ya meli hiyo kutokana na mvutano kati ya serikali ya Italia na Malta juu ya nani anawajibika kuchukua kundi hilo la watu.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa meli hiyo awali ilikuwa na wahamiaji 177 lakini baadhi yao wakiwemo watoto na wagonjwa waliruhusiwa kushuka kwenye meli na kuingia Italia.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo imeshukuru nchi ambazo zimekubali kuwapokea wahamiaji hao ambapo Ireland na Albania ni miongon mwa nchi zilizoripotiwa na vyombo vya habari kukubali kuwapokea.

Hali halisi inavyokuwa baada ya wasaka hifadhi na wahamiaji kuokolewa na boti za uokozi
UNHCR/Giuseppe Carotenuto
Hali halisi inavyokuwa baada ya wasaka hifadhi na wahamiaji kuokolewa na boti za uokozi

UNHCR imesema inaendelea kuomba kuwepo kwa mfumo maalum kwenye ukanda wa Mediteranea juu ya mpango wa kupokea wahamiaji au wakimbizi wanaookolewa baharini.

Kamishna Mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Fillipo Grandi amesema “tukio hili linapaswa kuwa ishara ya onyo. Wakimbizi na wasaka hifadhi wanaweka maisha yao hatarini ilhali serikali zinaendelea na mivutano ya kisiasa kwa suluhu za muda mrefu. Suala la Diciotti sasa limepatiwa jibu, lakini vipi iwapo kisa kingine kitatokea?”

Kwa mantiki hiyo Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR amesema kuna umuhimju wa ushirikiano wa uhakika miongoni mwa nchi za Muungano wa Ulaya kuhusu watu wanaookolewa baharini.

Mwaka huu pekee, ingawa idadi ya wasaka hifadhi Ulaya imepungua, bado zaidi ya watu 1600 wamekufa maji wakisaka kufika pwani za Ulaya.

UNHCR imesema iko tayari kusaidia nchi kuandaa mfumo wa kuokoa maisha na kushughulikia sababu za watu kukimbia makwao.

Idadi kubwa ya wahamiaji na wasaka hifadhi hao yaelezwa wanaotoka Eritrea.