Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la kisiasa lapitishwa ili kuchagiza hatua dhidi ya TB

Tedros Ghebreyesus, (kati) Mkurugenzi Mkuu wa WHO akihutubia kikao cha kwanza kabisa cha ngazi ya juu kuhusu TB ambacho kimepitisha azimio dhidi ya TB duniani. kushoto kwake ni Waziri wa afya wa Urusi na Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed
UN/Eskinder Debebe
Tedros Ghebreyesus, (kati) Mkurugenzi Mkuu wa WHO akihutubia kikao cha kwanza kabisa cha ngazi ya juu kuhusu TB ambacho kimepitisha azimio dhidi ya TB duniani. kushoto kwake ni Waziri wa afya wa Urusi na Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed

Azimio la kisiasa lapitishwa ili kuchagiza hatua dhidi ya TB

Afya

Viongozi wa nchi na wakuu wa serikali leo wamepitisha azimio la kisiasa lenye lengo la kuchagiza hatua dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, au TB unaosababisha vifo vya watu milioni 1.6 kila mwaka.

 

Likipatiwa jina “Ushirikiano wa kutokomeza TB:Hatua ya dharura ya kimataifa,” azimio hilo linalenga kusaka hatua ili hatimaye ugonjwa huo uwe  umetokomezwa ifikapo mwaka 2030, ukomo wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katika azimio hilo, viongozi hao wanasema wametambua changamoto zilizopo ikiwemo ukosefu wa vifaa, dawa sahihi na hata fedha, bila kusahau jinsi ambavyo TB inasababisha umaskini miongoni mwa familia, jamii na taifa.

Viongozi hao wanataja msingi wa azimio hili ni pamoja na “ kutambua kuwa usugu wa dawa za TB unakadiriwa kusababisha theluthi moja ya vifo vitokanavyo na usugu wa dawa duniani na kwamba malengo ya maendeleo endelevu yako mashakani kufikiwa iwapo tunashindwa kushughulikia tatizo la usugu.”

Ugonjwa wa Kifua Kikuu umelemaza utu wa binamu kwa miongo na bado unaendelea kutesa binadamu. “TB haifahamu mpaka, kila mtu yuko hatarini lakini unazidi kushamiri ambako kuna umaskini, utapiamlo au mapigano

Kwa mantiki  hiyo viongozi hao wameazimia pamoja na mambo mengine kutenga fedha zaidi za utafiti na kusaka dawa sahihi sambamba na kuhakikisha hakuna mtu yeyote mwenye TB ambaye hatofikiwa na upimaji na matibabu.

Kufuatia kupitishwa kwa azimio hilo lenye vipengele 53, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza  hatua hiyo akisema lina matarajio makubwa lakini mafanikio yake “yatawezekana iwapo tutaweka jitihada zetu kwenye takwimu bora na sayansi, maamuzi sahihi, kuwezesha jamii na hatua za kimkakati na zilizofadhiliwa.”

Wanawake wawili ambao wanapata matibabu ya kifua kikuu mjini Addis Ababa , Ethiopia.
The Global Fund/John Rae
Wanawake wawili ambao wanapata matibabu ya kifua kikuu mjini Addis Ababa , Ethiopia.

Kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu wake Amina J .Mohammed Katibu Mkuu amesema “ jukumu la Umoja wa Mataifa katika kutokomeza TB ni la dharura na kwamba gonjwa hili baya linagusa kila bara na kila nchi. Takribani watu milioni 10.4 wameambukizwa.”

TB imetajwa kuwa inachochewa na mizozo, njaa na umaskini huku mazingira hayo nayo yakitajwa kuchochea kuenea kwa ugonjwa huo hatari.

Ametaja changamoto kama vile usugu wa dawa akisema kila mwaka wagonjwa 600,000 wanakabiliwa na usugu wa tiba dhidi ya TB, “tunahitaji maendeleo ya kisayansi ili kupata mbinu bora zaidi za kukabiliana na TB, sambamba na tishio la ongezeko la usugu wa dawa za kuua vijiumbe maradhi.”

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kufuata mwongozo wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus na shirika lake katika kuchagiza usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwa serikali na mashirika ya kiraia na wadau wengine ili kupata kasi inayohitajika kutokomeza TB duniani.

Chanjo ya BCG ambayo hutumiwa dhidi ya Kifua Kikuu ikiwa inaandaliwa katika kituo cha afya Bougouni, Mali 2018.
© UNICEF/Ilvy Njiokiktjien
Chanjo ya BCG ambayo hutumiwa dhidi ya Kifua Kikuu ikiwa inaandaliwa katika kituo cha afya Bougouni, Mali 2018.

 

DKT. TEDROS NA OMBI LAKE KWA VIONGOZI

Mapema  Dkt. Tedros alieleza wajumbe kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu umelemaza utu wa binamu kwa miongo na bado unaendelea kutesa binadamu. “TB haifahamu mpaka, kila mtu yuko hatarini lakini unazidi kushamiri ambako kuna umaskini, utapiamlo au mapigano,” amesema.

Amegusia mpango waliozindua mapema mwaka huu wa kuhakikisha kuwa wanakuwa wametibu watu milioni 40 ifikapo mwaka 2022 akisema “tunaomba viongozi wa kisiasa waazimie kuwa mabingwa milioni 40 ili kusaidia kufikia lengo hili.”

Dkt. Ghebreyesus akataja mambo matatu amuhimu ambayo amesema yanaweza kusaidia kufikia lengo la kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030. “Mosi, tunahitaji msaada wenu usiotikisika. Tunaweza kufanikiwa tu iwapo tutaungwa mkono na viongozi wa  ngazi ya juu kabisa. Pili tunahitaji ongezeko la uwekezaji hasa katika sayansi na tafiti na tunahitaji dawa mpya, chanjo mpya na mbinu mpya za utambuzi wa TB.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO ametaja jambo la tatu kuwa ni kila mtu amwajibishe mwenzake. “Na ndio maana tunaandaa mfumo wa uwajibikaji ulio mtambuka ukiwa na misingi mikuu minne: Ahadi, hatua, ufuatiliaji na tathmini kuhakikisha kuwa kile tusemacho kinaenda sambamba na tunachotenda.”