Wakimbizi Warundi takribani 600 wamerejea nyumbani kwa hiari kutoka Tanzania

4 Oktoba 2019

Shirika la la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR na wadau kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania leo wamewasaidia wakimbizi takribani 600 wa Burundi kurejea nyumbani kama sehemu ya mpango wa wakimbizi kurudi nyumbani kwa hiari.

UNHCR imeitaka serikali ya Tanzania na Burundi kuhakikisha inaheshimu wajibu wao wa kimataifa wakati wa mchakato huo na kutomrejesha mkimbizi au muomba hifadhi yoyote kwa lazima.

“Tunaisihi serikali ya Tanzania na ya Burundi kuheshimu ahadi zao za kutekeleza matakwa ya kimataifa  ya kuhakikisha kila mkimbizi anarejea kwa hiari na kuwa hakuna mkimbizi au msaka hifadhi yeyote anayerejeshwa Burundi bila ridhaa yake.” Imesema UNHCR.

Aidha UNHCR imesema japokuwa haihimizi wakimbizi kurejea Burundi, iko tayari kuendelea kuwasaidia wakimbizi ambao wamefanya chaguao kwa hiari yao kurejea nchini mwao na pia itawasaidia katika kuhakikisha wanarejea katika Maisha ya kawaida  huko nchini Burundi.

Kwa mujibu wa takwimu za UNHCR, zaidi ya wakimbizi 76,000 wamesaidiwa kurejea nchini Burundi tangu Septemba 2017.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter