Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila mwalimu uwezekano wa kufanikisha lengo la elimu ni vigumu- Mwalimu Tabichi

Peter Tabichi wa Kenya, mshindi wa Tuzo ya kimataifa ya Mwalimu. Tabichi ni mwalimu wa sayansi ambaye anatoa asilimia 80 ya mshahara wake kusaidia watu maskini katika shule za vijijini Kenya
UN News/Grece Kaneiya
Peter Tabichi wa Kenya, mshindi wa Tuzo ya kimataifa ya Mwalimu. Tabichi ni mwalimu wa sayansi ambaye anatoa asilimia 80 ya mshahara wake kusaidia watu maskini katika shule za vijijini Kenya

Bila mwalimu uwezekano wa kufanikisha lengo la elimu ni vigumu- Mwalimu Tabichi

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuelekea siku ya walimu duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 5, Umoja wa Mataifa katika ujumbe wa pamoja wa mashirika yake umesema wakati dunia ikisherehekea siku ya walimu kuna pengo la walimu milioni 69 wanaohitajika katika kufikia lengo namba nne la malengo ya maendeleo endelevu , SDGs licha ya umuhimu wao katika kufanikisha lengo hilo.

Mmoja wa walimu ambao anachangia katika kufanikisha lengo hilo ni Mwalimu Peter Tabichi kutoka Kenya ambaye ni mwalimu wa somo la hisibati na fizikia katika shule ya sekondari ya Keriko iliyoko kaunti ya Nakuru. Mwalimu Tabichi pia  ni mshindi wa tuzo ya mwalimu bora kimatifa, katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili amezungumzia mchango wa mwalimu katika kufanikisha lengo la elimu kwa wote akisema, "Kwanza ukiangalia umuhimu wa elimu na umuhimu wa kuelimisha watoto, na ukitaja maswala ya maendeleo ni lazima kuzungumzia suala la elimu, na wakati ukizungumzia suala hilo ni lazima awepo mwalimu ambaye anafanya kazi kubwa katika kufanikisha upatikanaji wa elimu kwani analazimika kuandaa masomo mbali mbali na kusahihisha kazi ya ziada ikiwemo mitihani,"

Ameongeza kuwa kando na kufanikisha elimu kwa watoto, walimu pia wana kazi kubwa ya kusaidia kumkuza mtoto na kusema, "kazi ya mwalimu inakwenda mbali zaidi ya mazingira ya darasani kwani ni lazima mwalimu afuatilie kuhakikisha kwamba watoto wanakua katika mazingira sahihi huku wakiwa na nidhamu." Aidha ameongeza, "ni muhimu walimu wakatambulika kwa kazi kubwa wanayofanya licha ya kwamba wakati mwingi hawatambuliki."