Sikutaka kuolewa, nilitaka kusoma lakini ikashindikana:Habiba 

3 Januari 2020

Kutana na Habiba alimaarufu kama “Mama Solange” binti aliyelazimika kuacha shule na kuolewa akiwa na umri mdogo nchini Cameroon. 

 

Huyo ni Habina au Mama Solange binti mwenye umri wa miaka 17 kutoka nchini Cameroon  kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF aliolewa akiwa na umri wa miaka 14. Na baada ya baba yake kufariki dunia mama yake mzazi ambaye ni mlemavu wa kutoona alikuwa na changamoto kubwa ya kuisaidia familia yake na ndipo ndoto za shule za Habiba zikakatishwa ghafla.

“Mama yangu alinitaka kurudi nyumbani kuja kukutana na mtu nisiyemjua aliyekuja kututembelea, akisema alikuwa mjomba wetu wakati ukweli ni kwamba alikuwa mjomba wa muwe wangu. Na nilipofika wakafunga mlango. Kisha wakaita gari kunichukua na wakaondoka nami kwa shuruti. Nilitaka kuruka nje ya gari lakini kulikuwa na wanaume waliokuwa wakinilinda kila upande sikuweza kutoka.”

UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Asubuhi katika mitaa ya Melen, mtaa wa mabanda katikati ya mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé. Kwa muda mrefu Cameroon imekuwa katika mgogoro wa ndani.

Na huo ulikuwa mwanzo wa maisha ya ndoa ya Habiba japo hakuyataka kabisa“Siku hiyohiyo tulipowasili nilitaka kutoroka . Na kabla ya kutimiza wiki mbili nilifanikiwa kutoroka na kurudi nyumbani, lakini mama yangu akasema hapana siwezi kurudi na endapo nitafanya hivyo yeye ataondoka na kunilaani, ndio maana nikalazimika kurudi huko. Nilitaka kujiua.”

Mbali ya ndoa ya lazima Habiba alikuwa anapata kipigo mara kwa mara toka kwa mumewe ambaye alimzalisha akiwa bado mdogo “Nilikuwa na miaka 15 nilipopata ujauzito. Na mimba ilipokuwa na miezi saba alinipiga sana na tumbo likaanza kuniuma. Baada ya wiki moja bado nilikuwa na mauamivu wakanipeleka hospital ambako nilijifungua watoto mapacha wakiwa njiti”.

Na baada ya kujifungua mumewe akamtelekeza yeye na wanawe wachanga na hivyo akalazimika kurudi kuishi na mama yake mzazi, na wiki mbili baada ya kujifungua pacha mmoja alifariki dunia.

Nchini Cameroon msichana 1 kati ya 3 anaolewa kabla ya kutimiza miaka 18. Kwa sababu hiyo hivi sasa Habiba amekuwa mchagizaji wa kupinga ndoa za utotoni na kuielimisha jamii yake. Lengo kuu anasema anataka siku moja binti yake Anna Martha kwenda shule na kupata elimu.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud