Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa tunaona mkataba mpya Sudan Kusini ni wetu sote na si serikali pekee- Mkimbizi wa ndani

Alice Senna Philip, mwenyekiti wa kikundi cha wanawake jimboni Yei nchini Sudan Kusini akizungumza mbele ya ujumbe wa ngazi ya juu wa UNMISS ulioongozwa na mkuu wao David Shearer. Ujumbe huo ulitembelea eneo hilo.
UNMISS/Francesca Mold
Alice Senna Philip, mwenyekiti wa kikundi cha wanawake jimboni Yei nchini Sudan Kusini akizungumza mbele ya ujumbe wa ngazi ya juu wa UNMISS ulioongozwa na mkuu wao David Shearer. Ujumbe huo ulitembelea eneo hilo.

Sasa tunaona mkataba mpya Sudan Kusini ni wetu sote na si serikali pekee- Mkimbizi wa ndani

Amani na Usalama

Nchini Sudan Kusini harakati zinaendelea za kuhakikisha mkataba mpya wa amani uliotiwa sain mwezi Septemba mwaka jana huko Addis Ababa Ethiopia unakuwa na mashiko mashinani ili kila mtu aweze kushiriki na hatimaye amani ya kudumu na endelevu iweze kupatikana kwenye taifa hilo. John Kibego na ripoti kamili.

Miongoni mwa harakati hizo ni semina ya siku tatu inayofanyika kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, ikileta pamoja washiriki wapatao 60, kujadili kwa dhati jinsi ya kusongesha amani na changamoto wanazozipitia.

Washiriki ni viongozi wa kisiasa, kijadi, kidini na wawakilishi wa mashirika ya kiraia, jamii zilizofurushwa makwao, wanawake na vijana, wanawake na vijana.

Katika jukwaa hili lililoandaliwa na ujumbe wa  Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, baadhi ya washiriki wanaona fursa ya kujengeana imani na kushirikiana na jamii tofauti kama asemavyo TEresia Sirisio, Mwenyekiti wa chama cha Sudan African National Union.

Bi. Sirision amesema ya kwamba, “jukwaa hili kwa dhati ni ishara yetu ya kukubali, na kwamba tunaanza kujenga imani ili tuwe na amani Sudan Kusini. Nina matumaini makubwa kuhusu hili. Kuhusu jamii tofauti kuketi pamoja kwenye huu mkutano, nina imani na nina matumaini na jinsi tunashirikiana kama familia moja kwa lengo moja , hii ni amani.”

Akizungumza kwenye mkutano huu, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini na pia mkuu wa UNMISS, David Shearer amesema ni muhimu jamii zote nchini humo kushiriki kwenye mchakato wa amani na wakati huo huo kujenga mshikamano thabiti kuanzia mashinani hadi ngazi ya taifa.

Bwana Shearer amesema, "jukwaa la amani yetu ambalo tunashiriki leo, linatoa fursa muhimu kwa watu wa aina, uzoefu na utaalaamu mbalimbali kutumia ushawishi wao kuchagiza mchakato wa amani.”

Kwa upande wake, Rachel Mayik kutoka Malakal akiwakilisha wakimbizi wa ndani amesema, “nahisi warsha hii inaturuhusu kumiliki amani. Kama awali ambapo watu hawakushirikishwa, waliona amani ni ya wale waliotia saini kama vile serikali au kikundi cha SPLA upande wa upinzani na pande nyingine, lakini sasa kujumuisha mashina, wanahisi ni sehemu ya mkataba mpya.”