Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMAS  yategua mabomu huko Bor, wananchi wasema sasa watoto watacheza bila uoga

Kifaa cha kutegua mabomu kikisukumwa na gari maalumu
UNMAS
Kifaa cha kutegua mabomu kikisukumwa na gari maalumu

UNMAS  yategua mabomu huko Bor, wananchi wasema sasa watoto watacheza bila uoga

Amani na Usalama

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uteguzi wa mabomu ardhini UNMAS imebaini na kuondoa vilipuzi na mabomu ya kutegwa ardhini ambayo yalikuwa hayajalipuka kwenye eneo la Thon-Awai lililoko kilometa 5 kutoka mji wa Bor jimboni Jonglei.

Taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS imesema wakazi wa eneo hilo la Thon-Awai wamefurahishwa na hatua hiyo ya UNMAS ya kutegua mabomu hayo ambayo yaaminika yalitegwa kwenye eneo hilo wakati wa vita vya kusaka uhuru wa Sudan Kusini, na bila kuteguliwa yangalisababisha madhara yasiyofikirika.

Rebecca Morris anajisikia salama baada ya uteguaji wa mabomu uliofanywa na UNMAS
UNMAS
Rebecca Morris anajisikia salama baada ya uteguaji wa mabomu uliofanywa na UNMAS

Miongoni mwa wakazi hao ni Mary Aluel ambaye amesema “ninafurahi kuona mabomu hayo yameondolewa na tulikuwa hatujui kuwa yako hapa, sasa  tutalima bila wasiwasi na watoto wetu watacheza bila kuogopa kujeruhiwa.”

UNMAS bado inaendelea na kazi ya kubaini na kutegua mabomu na vilipuzi katika majimbo mengine nchini Sudan Kusini.

“Kuondoa vilipuzi hivi hatari kutoka kwenye ardhi ni kazi inayochocha na inayofanyika polepole na pia ina hatari kubwa,” imesema taarifa hiyo ya UNMISS ambapo mkuu wa ofisi ya ujumbe huo huko Bor,  Deborah Schein amepongeza kazi hiyo ya wateguaji mabomu akisema “wanafanya kazi hatari sana na muhimu kwa ajili ya kulinda raia kwenye jamii.”