Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipoteze muda na wasioamini kwenye mabadiliko ya tabianchi- Tanzania

Waziri wa Tanzania wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa  Mataifa kando mwa vikao vya mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York
Picha ya UN News/Patrick Newman
Waziri wa Tanzania wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando mwa vikao vya mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. (25 Septemba 2019)

Tusipoteze muda na wasioamini kwenye mabadiliko ya tabianchi- Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74, ukiingia siku ya nne hii leo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani, Tanzania imesema imetenga asilimia 32 ya eneo la nchi kama hifadhi ya misitu kama njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki  Profesa Palamagamba John Kabudi ametaja  hatua hiyo wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, kabla ya kuhutubia mkutano huo leo huku akizungumzia ombi la Katibu Mkuu wa UN la kuona nchi zinawekeza kwenye miradi rafiki kwa mazingira.

Profesa Kabudi amesema kwamba, “dunia imechelewa, wale ambao wamechangia kiasi kikubwa katika kuchafua mazingira na hivyo kuleta matatizo ya tabianchi. Wako ambao wanakana kwamba tatizo hilo halipo, hao tusipoteze muda wetu sana, lakini wale wanaokiri kwamba tatizo hilo lipo wajue kuwe pale wanapotoa fedha zao kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kushughulikia tatizo hilo katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hawafanyi hivyo kwa hisani bali wanatimiza wajibu wao. Wajibu wao kwa dunia hii ambayo wao kwa maendeleo yao ya viwanda yaliyotumia makaa ya mawe na mafuta na kuchafua dunia, sasa dunia iko katika hatari ya kuangamia, na wao wanapotoa fedha hizo hawatoi hisani. Ni haki yetu na wajibu wao kutoa hizo fedha. "

Kwa mantiki hiyo amesema kuwa, "kwa hiyo tunaungana kabisa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba nchi zetu zinazoendelea zinasaidiwa kupata maendeleo na wakati huo huo kuhifadhi mazingira. Na maana yake wote tuna wajibu wa pamoja wa kulinda mazingira, lakini kila mtu ana wajibu ulio tofauti. Wao waliochafua mazingira lakini sasa wana mali za kutosha, wana wajibu wa kutoa fedha, teknolojia ya kupambana na hiyo hali na sisi tuna wajibu wa kushiriki katika miradi hioy ili kunusuru na kuikoa dunia isiangamie mapema kuliko inavouytarajiwa."

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, Mavivi jimbo la kivu Kaskazini.
©MONUSCO/FIB/Mohammed Mkumba
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, Mavivi jimbo la kivu Kaskazini.

 

Kuhusu  kile ambacho Tanzania inataka kuona kwenye maeneo ya ulinzi wa amani  hususan kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako imepeleka askari kwenye kikosi maalum, Waziri Kabudi ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye UNGA74, amesema, “Tanzania ingependa muhula wa majeshi ya ulinzi wa amani ya MONUSCO uongezwe lakini ile brigedi ambayo Tanzania inashiriki ya kuhakikisha inapambana na magaidi na vikundi vyenye silaha ambayo vinaua watu kule DRC vinadhibitiwa . Na ili kufanya hivyo basi Tanzania inasema wakati imefika kwa Umoja wa Mataifa kuiwezesha hiyo bridgedi hiyo maalum kwanza kuwa na uwezo wa silaha au nyenzo za  kisasa ili iweze kupambana na vikundi hivyo vilivyojihami ."

Hata hivyo  Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema kuwa, "lakini wakati umefika sasa kuisaidia DRC kuwa na jeshi jipya na polisi mpya inayoweza kulinda amani kwenye maeneo  hayo, mpaka hali hiyo inafikiwa ya DRC kuwa na jeshi na polisi ya kulinda amani, nchi zote zina wajibu wa kusaidia DRC kuendelea kulinda amani na Tanzania iko tayari kuendelea kuwaweka askari wake DRC ili kuendelea kusaidia nchi hiyo na kuinusuru .”