UN: Asante Tanzania kwa ulinzi wa amani, Burundi sakeni suluhu ya janga la kisiasa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aendelea kuwa na mazungumzo na viongozi wanaowakilisha nchi zao kwenye mjadala mkuu wa UNGA74 na miongoni mwao ni kutoka Tanzania na Burundi.
Mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA74 ukiendelea kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi ambapo wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu pande mbili hizo.
Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa New York, alhamisi usiku imesema kuwa Guterres na Kabudi wamejadili hali inavyoendelea kwenye ukanda wa Maziwa Makuu ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Katibu Mkuu ameishukuru Tanzania kwa mchango wake wa kipekee kwenye ulinzi wa amani na kusisitiza utayari wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia juhudi za kitaifa za kukabiliana na misimamo mikali.
Bwana Guterres pia amekuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya nje wa Burundi Ezéchiel Nibigira ambapo Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kupata suluhu ya janga la kisiasa linaoendelea nchini humo wakati taifa hilo linaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Hata hivyo amesema suluhu hiyo ipatikane kwa njia ya mazungumzo huku akisisitiza kuunga mkono kwa kina usuluhishi unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.