Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo langu ni kuona vijana wanashiriki kilimo chenye tija na si bora kilimo - Mugo

Mkulima karibu na mji wa Kisumu nchini Kenya akilima shamba lake.
World Bank/Peter Kapuscinski
Mkulima karibu na mji wa Kisumu nchini Kenya akilima shamba lake.

Lengo langu ni kuona vijana wanashiriki kilimo chenye tija na si bora kilimo - Mugo

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Viongozi wa dunia wakikutana leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York Marekani kupitia azimio la kusongesha hatua kwa tabianchi, nchini Kenya vijana hivi sasa wanashiriki katika kilimo si tu chenye kuwawezesha kupata kipato bali pia kile kinacholinda na kuhifadhi mazingira lakini wanataka msaada zaidi ili waweze kusonga mbele.

Victor Mugo, kutoka mtandao wa vijana wa kilimo kinachojali mazingira nchini Kenya, ameelezea hayo wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani akifafanua kwanza  kile anachofanya..

(Sauti ya Victor Mugo)

Kazi yangu haswa ni kufanya kazi na vijana ambao wako kwenye ukulima, katika nchi yangu ninaona shida tatu kubwa ambazo zinakumba vijana au nchi yote. Kwanza ni ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na hili linasababisha shida nyingi zitokanazo na vijana kukosa ajira. Pili ni  ukosefu wa uhakika wa chakula, kuna baa la njaa ambalo linakumba nchi yangu mara kwa mara na hili linafanya watu kuwa na utapiamlo na la tatu ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yanakumba watu katika nchi yangu. Na katika kazi yangu nilifikiria kuhusu shida hizi tatu na kutafuta suluhisho. Kwa hiyo ninafanya kazi na vijana ili waweze kuingia kwenye kilimo, lakini kilimo ambacho kina tija na kinazingatia mabadiliko ya tabianchi.”

Kisha akaelezea ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huo wa viongozi wa dunia juu ya hatua kwa tabianchi unaofanyika leo hapa New York, Marekani.

(Sauti ya Victor Mugo)

“Mosi ni kwamba kuna msemo kuwa vijana hawataki kuingia kwenye kilimo, lakini kutokana na kazi yangu nimeona vijana wanataka kuingia kwenye kilimo lakini kilimo chenye faida. Kwa hiyo tunafaa kusaidia vijana waingie kwenye kilimo na si kilimo kisicho na tija, halafu vijana wenye tajriba kwenye kilimo wawe mfano kwa vijana wengine. La pili ni kuwaambia kuwa vijana wako katika mstari wa mbele katika kujihusisha na mambo ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa wanaona yanaathiri maisha yao, yanaathiri maisha yao ya usoni na wanataka kujihusisha na mambo ambayo yanasaidia kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Tatu,  ili kusaidia vijana kuingia kwenye kilimo chenye tija na kusaidia vijana kuingia kwenye harakati za kusaidia mabadiliko ya tabianchi, pia tungetaka Umoja wa Mataifa na nchi waweze kujihusisha na mambo ya vijana, tumeona vijana ambao wanajihusisha lakini hawana msaada wowote. Msaada unaweza kuwa fedha au mawazo ya jinsi ya kulima kilimo chenye tija, vijana wapate msaada ili kuhakikisha wanaendelea katika harakati hizo.”