Jacques Chirac afariki dunia, Guterres asema alikuwa mtetezi wa tabianchi

26 Septemba 2019

Rais wa zamani wa Ufaransa Jacques Chirac amefariki dunia hii leo ambapo kufuatia taarifa za kifo chake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema taifa hilo la Ulaya limepoteza mmoja wa viongozi wake muhimu waliokuwa mstari wa mbele kusongesha demokrasia ya ushirikiano wa kimataifa.

Akizungumza jijini New York Marekani hii leo kabla ya kuanza kuhubia mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu ufadhili kwa ajili ya maendeleo, Bwana Guterres amesema alifanya kazi na hayati Chirac kwenye Baraza la Muungano wa  Ulaya.

“Tulifanya kazi pamoja kwa miaka sita na nusu kama wafanyakazi wa Baraza la Muungano wa Ulaya na tuliendeleza urafiki wa kina,” amesema Bwana Guterres akisema kuwa, “napenda kutuma salamu zangu za rambirambi kwa mke wake na serikali ya Ufaransa pamoja na wananchi wake.”

Katibu Mkuu amerejelea kuwa anakumbuka kuwa wakati wa kikao cha ngazi ya juu cha wiki hii tabianchi ikiwa ni mada muhimu, Jacques Chirac alikuwa mwanzilishi wa dhati wa vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi siku nyingi zilizopita kwa kuweka suala hilo kama kitovu cha ajenda ya kimataifa

Hayati Chirac ambaye alikuwa Rais wa Ufaransa kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2007 amefariki dunia leo mjini tarehe 27 Septemba 2019 huko Paris, Ufaransa. Alikuwa na umri wa miaka 86.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud