Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN, Ufaransa na China kushirikiana zaidi kufanikisha ajenda ya tabianchi

Katibu Mkuu wa UN António Guterres, katika mkutano wa utatu na Ufaransa na China. Kushoto Waziri wa Mambo ya nje wa China, Wang Yi, na kati Waziri wa Mambo ya nje wa UFaransa Jean-Yves Le Drian.
UN Japan/Ichiro Mae.
Katibu Mkuu wa UN António Guterres, katika mkutano wa utatu na Ufaransa na China. Kushoto Waziri wa Mambo ya nje wa China, Wang Yi, na kati Waziri wa Mambo ya nje wa UFaransa Jean-Yves Le Drian.

UN, Ufaransa na China kushirikiana zaidi kufanikisha ajenda ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa pamoja na Ufaransa na China wamesisitiza ahadi yao thabiti ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo utekelezaji wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi.

Makubaliano hayo yamefikiwa huko Osaka, Japan hii leo, baada ya mazungumzo baina ya waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi, Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, mazungumzo yaliyofanyika kando mwa mkutano wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa na unaokuwa kwa kasi, G20.

Katika taarifa yao ya pamoja, pande tatu hizo zimekubaliana kuwa, “mabadiliko ya tabianchi yanatishia nchi zote duniani na hivyo kuna udharura wa kushirikiana na kuchochea utashi wa kisiasa ili kukabili kwa pamoja tishio hilo.”
 
Halikadhalika wameelezea utayari wao wa kutekeleza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi kwa misingi ya uwiano unaozingatia wajibu na uwezo wa kila nchi na mazingira ya kila taifa.

Miradi ya kiasili ifadhiliwe 

Mkutano wa utatu kuhusu tabianchi baina ay Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres na mawaziri wa mambo ya nje wa China na Ufaransa
UN Japan/Ichiro Mae.
Mkutano wa utatu kuhusu tabianchi baina ay Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres na mawaziri wa mambo ya nje wa China na Ufaransa

China, Ufaransa na Umoja wa Mataifa pia wamesisitiza umuhimu wa kufadhili miradi ya kiasili ya kukabili mabadiliko ya tabianchi wakisema kuwa ina faida kubwa katika kupunguza makali na inajenga mnepo.
 
Kuhusu suala la kila nchi kutimiza ahadi kwa mujibu wa  mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, pande hizo tatu zimesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuna fedha kila wakati zinazoelekezwa kwenye miradi ya kukabili mabadiliko  ya tabianchi.
 
Wamerejelea pia suala la kuhakikisha nchi zilizoendelea zinatimiza ahadi zao za kutenga dola bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya kusaidia mataifa maskini kutekeleza miradi ya mazingira.
 
Wakiangazia mabadiliko ya tabianchi na ajira, pande tatu hizo zimesisitiza umuhimmu wa uanzishaji wa fursa za ajira ambazo ni za utu, za hali ya u una zinazosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira sambamba na kusaidia umma kufanikisha malengo ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.
 

Vifaa vinavyotoa hewa chafuzi navyo viondolewe

Ni katika mazungumzo hayo, Ufaransa na China zimearejelea ahadi yao ya kuridhia na kutekeleza itifaki ya Kigali na itifaki ya Montreal10 na kusaidia kuboresha uondoaji wa vifaa vinavyotoa hewa chafuzi za HFCs zinazotoboa tundu la ozone.

Mapema akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu amerejelea kauli yake ya kwamba, “sasa tunakabiliwa na hali nyingine mbaya. Tunaona vitu duniani kote vikienda shaghalabaghala kuliko tulivyotarajia.”


Kwa mantiki hiyo amesisitiza ushirikiano wa kimataifa ili kukabili mabadiliko  ya tabianchi na hivyo kuondokana na majanga ya sasa kama vile ukame, vimbunga na joto la kupindukia.