Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

‘Mkono kwa mkono’ kunusuru njaa katika nchi maskini- FAO

Mkakati wa FAO wa kusaidia kukabiliana na njaa kwenye bonde la Ziwa Chad umeleta nuru kwenye uhakika wa chakula.
FAO/Pius Utomi Ekpei
Mkakati wa FAO wa kusaidia kukabiliana na njaa kwenye bonde la Ziwa Chad umeleta nuru kwenye uhakika wa chakula.

‘Mkono kwa mkono’ kunusuru njaa katika nchi maskini- FAO

Masuala ya UM

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema kitendo cha nchi wanachama wa Umoja waMataifa kusaidia na kuunga mkono harakati za shirika hilo kama mpango mpya wa Mkono kwa Mkono,  kitaasaidia kuchagiza mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs hususan lile la kutokomeza njaa, na hivyo kutomwacha nyuma mtu yeyote.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema hayo katika  ujumbe wake kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kando katika moja ya vikao vinavyoendelea kando ya mjadala mkuu wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Kikao hicho kilikuwa kinajadili ili kuibuka na dira mpya ya kuwa na mbinu mpya bunifu za FAO zenye lengo la kuimarisha ubia kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea.

Miongoni mwao ni mpango wa Mkono kwa Mkono ambao ulitambulishwa kwenye kikao hicho ukilenga kuleta pamoja nchi zenye viwango vya juu vya njaa na umaskini na zile tajiri ili kusaidia juhudi za maendeleo hususan za nchi zisizo na bandari, visiwa vidogo maskini na nchi zilizoathiriwa na baa la njaa.

Baada ya hapo, mpango huo utalenga kusaidia nchi zenye idadi kubwa ya watu na zile maskini.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO amesema mpango huo utatekelezwa kwa uratibu na ubia wa karibu na benki za kimataifa za maendeleo na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa huku FAO ilibainisha fursa katika ngazi ya taifa kwa mataifa yote husika, sambamba na vikwazo na pengo la uwekezaji na kuandaa muundo wa kina wa ufuatiliaji na tathmini ukiwa na malengo dhahiri kwa mwaka 2030.

Bwana Qu Dongyu amesisitiza kuwa mikakati hiyo mipya “pia inalenga kuimarisha FAO ya kidijitali na iliyoimarika ambayo inaweza kuaminiwa na nchi wanachama na mfumo huu unalenga katika ubia, uwazi na sera za uwazi.”

“Hebu na tuimarishe ubia, tujenge kuheshimiana na kuaminiana na tuimarishane kupitia lengo letu la pamoja la kufanikisha SDGs na kuwa na dunia isiyo na njaa,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO.