Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika ina mengi ya kujifunza kupitia ufahamu na tamaduni za ulaji za wajapani- FAO

Ushirika wa mataifa ya Kusini-SSC- yanatoa mafunzo ya maelekezo kuhusu ulimaji wa mpunga Cote D'ivoire.
©FAO/Wang Jinbiao
Ushirika wa mataifa ya Kusini-SSC- yanatoa mafunzo ya maelekezo kuhusu ulimaji wa mpunga Cote D'ivoire.

Afrika ina mengi ya kujifunza kupitia ufahamu na tamaduni za ulaji za wajapani- FAO

Utamaduni na Elimu

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema mataifa ya Afrika yanaweza kunufaika zaidi kutokana na ufahamu na utamaduni wa Japani katika ulaji wa vyakula vyenye afya na lishe, amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Qu Dongyu. 

Bwana Qu, katika ziara yake ya kwanza kabisa nchini Japan tangu ashike wadhifa wa ukurugenzi Mkuu wa FAO amesema taifa hilo la Asia Mashariki lina teknolojia janja, mashine za kisasa za kilimo na mbinu bora za masoko sambamba na viwango vya juu vya chakula na usalama wa chakula.

Ni kwa mantiki hiyo Mkurugenzi Mkuu huyo ametoa shukrani zake kwa ushirikiano kati ya FAO na Japan barani Afrika, ushirikiano ambao amesema umesaidia kuendeleza minyonyoro fanisi na jumuishi hasa kwenye kilimo cha mpunga na uimarishaji wa biashara ndogo na za kati.

"Tunaendelea kutegemea ukarimu wa Japan katika kuongeza usaidizi wake kwenye kuimarisha lishe barani Afrika,” amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO wakati akizungumza kwenye tukio la ushirikiano mpya wa kiuchumi kwa maendeleo ya Afrika, NEPAD na shirika la ushirikiano wa kimataifa la Japan, JICA, huko mjini Yokohama nchini Japan.

Tukio hilo lililenga kuangazia mpanog wa kuimarisha uhakika wa chakula na lishe barani Afrika, IFNA ambapo Bwana Qu amewaeleza viongozi wa Afrika na mawaziri wa kilimo kutokomeza njaa na aina zote za utapiamlo barani Afrika vinasalia kuwa kipaumbele cha FAO.

Amesisitiza umuhimu wa IFNA katika kufanikisha malengo hayo ya kutokomeza njaa kupitia mbinu za kuwezesha wakulima kupata vyakula vyenye lishe bora kwa kuwekeza kwenye kilimo, mifumo ya usimamizi, ubia kati ya sekta binafsi na ya umma na teknolojia na ubunifu.