Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Lori linapakua nafaka katika kiwanda cha kusindika nafaka nchini UkrainE.

G7: FAO yatoa mapendekezo ya kukabiliana na uhaba wa chakula wa sasa na ujao

© FAO/Genya Savilov
Lori linapakua nafaka katika kiwanda cha kusindika nafaka nchini UkrainE.

G7: FAO yatoa mapendekezo ya kukabiliana na uhaba wa chakula wa sasa na ujao

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO Qu Dongyu ametoa wito kwa nchi tajiri zaidi duniani G7 kusaidia kukabiliana na uhaba wa chakula katika siku zijazo kwani vita inayoendelea nchini Ukraine imepunguza usambazaji na kupandisha bei juu katika viwango vya kuvunja rekodi na kuyaweka mashakani mataifa ambayo tayari yana hatari ya kuathirika kote barani Afrika na Asia.

Akizungumza katika mkutano wa G7 uliofanyika leo huko Stuttgart  nchini Ujerumani kwa mualiko wa rais wa G7 Cem Özdemir  ambaye ni Waziri wa kilimo wa Ujerumani uliojadili Mzozo wa vita barani ulaya Mashariki  na Uhakika wa Chakula Duniani Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO amesema “Tunahitaji kutambua kikamilifu njia za kufidia mapungufu yanayoweza kutokea katika siku zijazo katika masoko ya kimataifa, tukifanya kazi pamoja ili kukuza ongezeko la uzalishaji endelevu inapowezekana.”

Vita ya Ukriane na Urusi iliyoanza mwezi Februari 2022 imeathiri dunia katika mazao ya ngano, mahindi, mafuta na mbolea kwakuwa nchi hizo zinachangia kiasi kikubwa cha usambazaji wake duniani. 

Qu amezitaja nchi ambazo zinategemea sana uagizaji wa ngano ni pamoja na Misri na Uturuki, lakini pia nchi kadhaa zilizoko katika ukanda wa jangwa la Sahara kama vile Congo, Eritrea, Madagascar, Namibia, Somalia na Tanzania.  
Wakati huo huo, nchi ambazo zinategemea sana mbolea inayoagizwa kutoka Urusi ni Argentina, Bangladesh na Brazil.

Nchi zenye nyota zinategemea uagizaji wa chakula kutoka Ukraine na Urusi.
FAO
Nchi zenye nyota zinategemea uagizaji wa chakula kutoka Ukraine na Urusi.

Nini Kifanyike

Mkuu huyo wa FAO ametaja mambo kadhaa ambayo iwapo yakifanyika yatasaidia si kupunguza uhaba wa chakula kwa muda mfupi pekee bali kuimarisha nchi hadi siku za usoni

Uwazi wa soko ni muhimu- FAO inakaribisha kila juhudi za kuimarisha na kupanua Mfumo wa Taarifa za Soko la Kilimo -AMIS ili kuongeza uwazi wa soko la chakula lililozinduliwa mwaka 2011 na Mawaziri wa Kilimo wa G20 kufuatia kupanda kwa bei ya chakula duniani mwaka 2007/08 na 2010. (AMIS inasimamiwa na FAO)

Mfumo wa Kimataifa wa Kufadhili Uagizaji wa Chakula- FAO imependekeza mfumo huu ili kusaidia mataifa kukabiliana na kupanda kwa bei ya vyakula. Utaratibu huo, ambao unategemea mahitaji na ukomo kwa nchi za kipato cha chini na cha kati, zinazoagiza chakula kutoka nje na walengwa waliochaguliwa wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa, unaweza kunufaisha karibu watu bilioni 1.8 katika nchi 61 zilizo hatarini zaidi duniani.

Ameleza kuundwa kwa Kituo ili kujumuisha masharti mahiri na kufanya kazi ya kujiendesha chenyewe kwa ufadhili wa siku za usoni. Nchi zinazostahiki zitajitolea kuongeza uwekezaji katika kilimo, na hivyo kupunguza mahitaji ya uagizaji wa siku zijazo.

Katika hotuba yake kwenye mkutano huo wa G7, Mkurugenzi Mkuu wa FAO pia alitoa wito kwa serikali "kujizuia kuweka vikwazo vya kuuza nje, ambavyo vinaweza kuzidisha ongezeko la bei ya chakula na kudhoofisha imani katika masoko ya kimataifa."

Qu akitoa takwimu za hali ilivyo duniani amesema mwaka  2021, takriban watu milioni 193 walikuwa na uhaba wa chakula na wanahitaji msaada wa haraka hili likiwa ni uongezeko la takriban watu milioni 40 kutoka mwaka 2020.

"Ni katika muktadha huu wa kushangaza ambapo sasa tunakabiliwa na vita nchini Ukraine," alisema Qu.