Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwazi, haki na usawa ndio utakuwa msingi wa uongozi wangu: Qu Dongyu

Mkurugenzi mkuu mteule wa FAO , Dkt. Qu Dongyu wakati akihutubia kikao cha 41 cha shirika hilo mjini Roma Italia baada ya kutangazwa kuwa mshindi . Pichani akiwa jukwaani na mkurugenzi mkuu wa sasa wa FAo Jose Graziano da Silva (23 Juni 2019)
FAO/Alessandra Benedetti
Mkurugenzi mkuu mteule wa FAO , Dkt. Qu Dongyu wakati akihutubia kikao cha 41 cha shirika hilo mjini Roma Italia baada ya kutangazwa kuwa mshindi . Pichani akiwa jukwaani na mkurugenzi mkuu wa sasa wa FAo Jose Graziano da Silva (23 Juni 2019)

Uwazi, haki na usawa ndio utakuwa msingi wa uongozi wangu: Qu Dongyu

Masuala ya UM

Mkurugenzi mkuu mteule wa shirika la chakula na kilimo FAO,  Dkt. Qu Dongyu amesema uwazi, haki na usawa hususuani kwa walio mashinani ndio itakuwa nguzo ya uongozi wake. Dkt. Dongyu ameyasema hayo wakati wa kikao cha 41 cha FAO kilichomtangaza rasmi kuwa mshindi wa nafasi hiyo mjini Roma Italia.

Dkt. Ndongyu atakuwa mkurugenzi mkuu wa tisa wa shirika hilo tangu lililipoanzishwa 16 Oktoba 1945. Muhula wake mkurugenzi huyu mpya kutoka China utaanza rasmi 1 Agosti 2019.

Akizungumza kwenye makao makuu ya shirika hilo mjini Roma Italia mara tu baada ya kutangazwa rasmi kuwa ndiye atakaye mrithi Jose Graziano da Silva kuendesha gurudumu la FAO Dkt. Ndogyu amesema “Siku ya leo ni siku muhimu sanan a ni siku yenu nchi wanachama, katika kusongesha mbele ajenda ya maendeleo endelevu SDGs. Nawashukuru sana kwa kuniunga mkono katika kubeba kijiti hiki na kuweka mikakati ya mustakbali wa FAO na kazi zake.” Ameishukuru pia familia yake kwa kusimama naye katika mchakato huu lakini pia nchi yake na wafanyakazi wote wa FAO ambao atafanya nao kazi.

Ameongeza kuwa “Kama mkurugenzi mkuu mteule mpya wa FAO nitazingatia misingi na kanuni za FAO hasa kuhakikisha haki, uwazi na usawa, nitafanya kila niwezalo kuhakikisha nchi wanachama hususan wakulima wanafanya kazi kwa pamoja na FAO kusongesha ajenda hiyo ya maendeleo.”

Naye mkurugenzi mkuu anayemaliza muda wake Jose Graziano da Silva amepongeza Dkt. Dongyu pamoja na watu wa Jamhuri ya China kwa kuchaguliwa kwake na kumkabidhi kijiti akisema “hongera sana Dkt. Dongyu na watu wa China kwa kuchaguliwa kwako na nakutakia kila la heri katika utendaji kazi wako.”

Da Silva atan’gatuka rasmi Julai 31 baada ya kuongoza shirika hilo kwa miaka minane tangu Januari Mosi mwaka 2012.