Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa amani Sudan Kusini unahitaji u tayari wa pande husika na msaada wa jamii ya kimataifa-Shearer

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer akihutubia Baraza la Usalama.
UN Photo/Ariana Lindquist
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer akihutubia Baraza la Usalama.

Mchakato wa amani Sudan Kusini unahitaji u tayari wa pande husika na msaada wa jamii ya kimataifa-Shearer

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer amesema mchakato wa amani nchini humo unasalia kuwa, “hatarini, lakini hatua zinapigwa, ” akiongeza kuwa hatua zinategemea u tayari wa pande husika na uungwaji mkono na jamii ya kimataifa katika kuunda serikali ya mpito.

Bwana Shearer ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja nwa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS amesema hayo wakati akihutubia Baraza la Usalama leo Jumatano jijini New York, Marekani kuhusu hali nchini Sudan kusini ikiwa ni siku sita tu baada ya maadhimisho ya kwanza tangu kutiwa saini kwa mkataba ulioboreshwa wa kutatua mzozo wa Sudan Kusini.

Akizingatia kwamba ziara ya hivi karibuni huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini ya Riek Machar kwa mwaliko wa Rais Salva Kiir ilikuwa ni hatua muhimu kwa ajili ya mchakato wa amani, Shearer amesema kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji hatua zaidi.

Bwana Shearer ameliambia Baraza la Usalama kwamba, “mpango wa pamoja wa sekta ya usalama unahitajika,’ akiongeza kwamba UNMISS imetafuta msaada wa jenerali kutoka ukanda huo kwa ajili ya kusaidia pande husika kufuatilia sera za kiusalama ikiwemo ukubwa na muundo wa vikosi.”

Aidha Mkuu huyo wa UNMISS amerejelea kusema kwamba, “uundwaji wa serikali ya mpito unatoa fursa ya kuinua macho yetu kutoka changamoto za sasa hivi na kutazama siku za usoni kuelekea uchaguzi unaotarajiwa baada ya miaka mitatu ya serikali ya mpito.

Ameongeza kwamba, “uchaguzi unatoa fursa ya kutatua tofauti kupitia njia ya kidemokrasia kuliko njia za kikatili, na kutokana na mfumo wa majadiliano yanayofanya kati ya watu wenye hadhi na kuwasilisha sera kwa serikali iliyoteuliwa na watu.”

Mwakilishi huyo maalum amezingatia kwamba kufanyika kwa uchaguzi huru na wa hakai si suala tu la kujiandaa kivifaa bali kunahitaji kuwepo kwa fursa ya kisiasa ambako kwamo vyama vya kisiasa vinaweza kutunga na kujadili sera na kufanya kampeni kwa uhuru.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa Balozi, Akuei Bona Malwal amesema kwamba mkutano kati ya Rais  Kiir na Bwana Machar ulikuwa ni majadiliano kuhusu namna ya kutekeleza makubaliano yaliyoboreshwa ya amani na kikubwa ni kwamba serikali hiyo inapaswa kuundwa kufikia mwezi Novemba 12 mwaka huu wa 2019.