UM walaani mauaji Sudan Kusini

Picha: UM/Tim McKulka
Walinda amani wa UNMISS wapiga doria Jonglei nchini Sudan Kusini.

UM walaani mauaji Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya raia na utekaji nyara wa wanawake na watoto kwenye jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini.

Yaripotiwa kuwa watu waliojihami waliua raia zaidi ya 40 siku ya Jumanne na kuteka nyara wanawake na watoto kwenye eneo la Duk Payel.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa umoja huo nchini Sudan Kusini, David Shearer amesema..

(Sauti ya David Shearer)

“Nalaani mauaji haya na utekwaji nyara wa wanawake na watoto 60 ulioambatana na mashambulizi haya. Nasihi jamii zote kujizuia ili kuondokana na mfululizo wa mauaji ya kulipiza kisasi ambayo yameshamiri sana kwenye sehemu hii ya nchi. Ni muhimu kwa mamlaka za jimbo na nchi kushirikiana ili kuwafikisha mbele ya sheria watekelezaji wa kitendo hiki.”

Bwana Shearer ambaye ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS amesema kwa upande wao watafanya kila wawezalo kujaribu kuleta amani kwenye eneo hilo na kusaidia jamii ambazo ziko tayari kufuata mkondo wa amani.