Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shehena yenye misaada ikitua visiwa vya Bahama, UNICEF yahitaji dola milioni 4.

Benson Etienne mwenye umri wa miaka 15 na familia yake walikimbia makazi yao kabla nyumba yao haijabomolewa na kimbunga dorian huko eneo la bandari ya March, kisiwa cha Abaco nchini Bahama
© UNICEF/Moreno Gonza
Benson Etienne mwenye umri wa miaka 15 na familia yake walikimbia makazi yao kabla nyumba yao haijabomolewa na kimbunga dorian huko eneo la bandari ya March, kisiwa cha Abaco nchini Bahama

Shehena yenye misaada ikitua visiwa vya Bahama, UNICEF yahitaji dola milioni 4.

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema linatahija dola milioni 4 za dharura ili kusaidia mahitaji ya haraka ya watoto na familia zao huko visiwani Bahama baada ya kimbunga Dorian kupiga eneo hilo na kusababisha madhara makubwa.

Kwa mujibu wa UNICEF, dola hizo milioni 4 zinalenga kufanikisha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za kujisafi, lishe, misaada ya kisaikolojia na elimu.

Ombi hilo la UNICEF linakuja wakati huu ambapo ndege iliyosheheni tani 1.5 ya misaada ya dharura ya kuokoa maisha iliwasili jana kwenye mji mkuu wa visiwa vya Bahama, Nassau.

Vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na vidonge 400,000 vya kutakatisha maji, matenki kadhaa ya ujazo wa lita 5,000 za maji na madumu 1,000 ya kutekea maji, vinalenga kusaidia zaidi ya watoto 9,500 na familia zao kupata maji safi na salama kufuatia kimbunga Dorian kilichosambaratisha miundombinu ya maji nchini humo.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo huko New  York, Marekani, Panama City, Panama na Nassau, Bahama imesema kuwa shehena hiyo ni ya kwanza kupelekwa na shirika hilo na ilisafirishwa na ndege ya shirikisho la msalaba mwekundu na hilal nyekundu, IFRC na vinatarajiwa kuanza kusambazwa kwa jamii siku chache zijazo.

Takribani watoto 18,000 kwenye kisiwa cha Abaco na kisiwa cha Bahama Kuu wameathiriwa na kimbunga Dorian ambapo wengi wao wanahitaji misaada ya kibinadamu, na makadirio hayo ni kwa mujibu wa mamlaka ya dharura za majanga ya Karibea, CEDMA.
 
Siku y aIjumaa, UNICEF iliweza kufika eneo la Abaco, eneo ambalo limeathiriwa zaidi na kimbunga Dorian kilichopiga visiwa vya Bahama wiki mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo maafisa wa shirika hilo walishuhudia uharibifu mkubwa shule zikiwa zimesambaratishwa, halikadhalika hospitali, nyumba, barabara huku magari na mashua vikiwa vinanin’ginia kwenye miti.
 
“Watoto na familia zao ambao wamenusurika kwenye kimbunga hiki wamepoteza nyumba zao, mbinu zao za kuishi, ndugu na jamaa na wamesalia na kiwango kidogo cha maji na chakula,”
amesema Youssouf Abdel-Jelil, Naibu Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Amerika ya Kusini na Karibea.

Bwana Abdel-Jelil amesema muda unakwenda kwa wao kupata misaada akisema kuwa siku tano tangu kimbunga hicho kipige eneo hilo, maji safi na salama ni kitu kinahitajika zaidi sambamba na vifaa vya dharura kwa ajili ya akina mama na watoto.