Mahitaji ya chakula yamefikiwa, kipaumbele sasa ni msaada wa vifaa-WFP

10 Septemba 2019

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linasaidia harakati za kutoa msaada wa dharura  Bahamas nchi ambayo inakabiliwa na athari kubwa zilizosababishwa na kimbunga Dorian, ikiwa ni kimbunga kibaya zaidi kuwahi kukumba visiwa hivyo.

Akizungumza na waandihsi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa WFP Herve Verhossel amesema WFP imewasilisha vifaa vya hifadhi, jenereta na vifaa vya ofisi ambapo inatarajia kutengeneza kituo cha kuratibu mipango ikiwemo kuwezesha kuwasili, uhifadhi na usafirishaji wa bidhaa za msaada lakini piakuhakikisha utaratibu wa misaada katika visiwa hivyo.

Kufikia sasa WFP imesambaza milo iliyo tayari 1,500 huku chakula kikifikia watu walio katika maeneo magumu kufikia katika visiwa vidogo vya Abaco ambakobwana Verhossel amesema,

“Kwa mujibu wa tathmini za hivi karibuni, mahitaji ya chakula ya sasa yamefikiwa kufuatia huduma ya watoa misaada ya kibinadamu walioko mashinani. Kwa mantiki hiyo, WFP litajikita na uratibu na msaada wa mawasiliano kwa ajili ya juhudi za msaada.”

Asilimia 90 ya nyumba na miundombinu katika visiwa vya Abaco imeharibiwa huku nyumba nyingi zikikosa umeme.

Timu za ufuatiliaji ikiwemo wafanyakazi wa WFP wanaendelea kufikia maeneo yaliyotengwa hatahivyo baadhi ya maeneo katika visiwa vya Grand Bahama na Abaco vinafikiwa baadhi ya maeneo bado ni vigumu kuyafikia.

Kufikia sasa serikali ya Bahamas kwa kushirikiana na msaada wa ndege za kijeshi, za kiraia na boti wamehamisha watu takriban elfu tano kutoka visiwa vilivyoathiriwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud