Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani na China wagawana manufaa ya uchumi wa kidijitali duniani, Afrika yajikongoja- Ripoti

Vijana wakitumia kompyuta mjini Kampala, Uganda.
World Bank/Arne Hoel
Vijana wakitumia kompyuta mjini Kampala, Uganda.

Marekani na China wagawana manufaa ya uchumi wa kidijitali duniani, Afrika yajikongoja- Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya iliyotolewa leo na Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema kuwa ukosefu wa usawa duniani utaendelea hadi pale pengo kati ya nchi zilizo mbele kimtandao na zile zisizo na mtandao litakaposhughulikiwa.

Ikiwa ni ya kwanza kabisa ikiangazia uchumi utokanao na huduma za kidijitali, ripoti hiyo imeweka bayana manufaa yatokanao na chumi zilizounganika zaidi kimtandao lakini inataka juhudi zaidi za pamoja ili manufaa hayo yaweze kunufaisha pande zote.

Marekani na China zasonga mbele, Afrika na Amerika ya Kusini zajikongoja

Ripoti inazitaja Marekani na China kuwa ndio zinanufaika zaidi na uchumi wa kidijitali, ambapo mataifa hayo mawili yanagawana asilimia 75 ya hataza zote zinazohusiana na teknolojia za miamala bila kuhitaji huduma za kibenki.

Halikadhalika zinanufaika kwa asilimia 50 ya mapato ya biashara za kiintaneti na zaidi ya asilimia 75 ya soko la kuweka takwimu kwenye mitandao.

Marekani na China zikinufaika zaidi na uchumi wa kidijitali, bara la Afrika na nchi za Amerika ya Kusini zinajikongoja.

Ripoti hiyo inasema kuwa kwa maeneo mengine, hususan Afrika na nchi za Amerika ya Kusini, bado zinajikongoja na iwapo mwelekeo huu utaendelea, utazidi kusababisha zaidi ukosefu wa usawa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye dibaji ya ripoti hiyo.

 “Tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa pengo la kidijitali katika dunia ambayo nusu ya dunia ina mkwamo kwenye mtandao wa intaneti au haina kabisa mtandao huo. Ujumuishi ni muhimu katika kujenga uchumi wa kidijitali ambao unanufaisha kila mtu,” amesema Guterres.

Matumizi ya takwimu yameongezeka

Licha ya manufaa yaliyodhihirika ya takwimu za kidijitali, ripoti inasema bado ulimwengu haujaweza kuwa mstari wa mbele wa kuwa na uchumi unaochochewa au kusongeshwa kwa data hizo.

Hata hivyo ripoti inakadiria kuwa kwa siku zijazo kutakuwepo na ongezeko kubwa  la mwenendo wa takwimu katika miaka michache ijayo.

“Hii inadhihirishwa na ongezeko la idadi ya watu wanaotumia mtandao wa intaneti, na teknolojia za kisasa zaidi za uchambuzi wa data, akili bandia, uchapishaji wa utatu, maroboti na uwekaji wa data kwenye kompyuta,” imesema ripoti hiyo.

Malipo ya miamala kwa njia ya kidijitali yanatumika sasa kuinua uchumi wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Afrika
Benki ya Duniak/Simone D. McCourtie
Malipo ya miamala kwa njia ya kidijitali yanatumika sasa kuinua uchumi wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Afrika

Majukwaa ya kutawala dunia

Utajiri na nguvu kwenye nyanja za kidijitali vinazidi kushikiliwa na majukwaa ya kisasa na machache yakihusisha kampuni za saba za kimataifa ambazo ni Microsoft, Apple, Amazon, Google, Facebook, Tencent na Alibaba.

Ripoti inasema kati ya hizo, kampuni hizo zinamiliki soko lenye thamani ya asilimia 70: Nchini China kuna WeChat ikimilikiwa na Tencent, huku  AliPay, ambayo ni kampuni ya Alibaba imekamata soko la malipo ya simu nchini China.

Google nayo inamiliki asilimia 90 ya soko la intaneti ilihali Facebook inamiliki jukwaa la mtandao wa kijamii katika zaidi ya asilimia 90 ya mataifa.

Ripoti inaonesha kuwa kampuni hizi zinashindana kwa kiasi kikubwa ili ziweze kusalia kileleni kwa kununua washindani wao, kupanua huduma zao, kusaka watunga sera na kuanzisha ubia mpya na kampuni za kimataifa zilizokuwa zimezoeleka awali.

UNCTAD inaonya kuwa kitendo cha majukwaa haya kujinasibu yao yenyewe kunasababisha kujikita eneo moja kwa thamani ya kidijitali na badala ya kupunguza ukosefu wa usawa kati na baina ya nchi huku nchi zinazoendelea zikisalia za mwisho.

Ripoti inataka fikra ambazo zitaleta mgawanyo sawa wa mapato yatokanayo na uchumi wa kidijitali.

Arnold Kayanda/UNNewsKiswahili
Tunataka dijitali iwe ya manufaa badala ya kuongeza matatizo-Nanjira Sambuli

Jukumu la serikali katika kusawazisha hali ya sasa

Serikali zina jukumu muhimu katika kuainisha upya kanunu za biashara, ameeleza Katibu Mkuu wa UNCTAD Mukhisa Kituyi akisema ni “kwa kuweka sheria za sasa ziendane na mazingira ya sasa na kupitisha mpya katika maeneo mengi.”

“Ukumbatiaji bora wa teknolojia mpya, kuimarisha ubia na uongozi bora vinatakiwa ili kupatia ainisho jipya mikakati ya kiteknolojia na  mwelekeo mpya wa utandawazi,” ameandika Dkt. Kituyi katika ripoti hiyo.

Ripoti inataka ushirikiano zaidi wa kimataifa kwenye suala hilo la  uchumi wa kidijitali,kwa kushirikisha ipasavyo mataifa yanayoendelea kwenye masuala kama vile ushindani, utozaji ushuru, usafirishaji wa data baina ya mipaka, hakimiliki na sera za biashara na ajira.