Elimu ya wakimbizi iko katika janga-UNHCR

Zaidi ya nusu ya watoto wakimbizi milioni 7.1 wa umri wa kwenda shule hawaendi shule, ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR iliyotolewa leo imebainisha. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.
Ripoti hiyo iliyopewa jina Ongezeko: Elimu ya wakimbizi katika janga, inaonesha kuwa kwa kadri watoto wakimbizi wanavyozidi kukua, ndivyo vikwazo vinavyowazuia kutopata elimu vinavyozidi kuwa vigumu kuvivuka. Melissa Fleming, msemaji wa kamishna mkuu wa UNHCR anasema, “Ni asilimia 63 ya watoto wakimbizi ambao wanaenda katika shule ya msingi ikilinganishwa na asilimia 91 kidunia. Inakuwa vibaya zaidi unapofikia ngazi ya sekondari ni asilimia 24 tu ya wakimbizi hupata fursa hiyo ikilinganishwa na asilimia 84 kidunia.”
Kamishna mkuu wa UNHCR Filippo Grandi anasema, “shuleni ni mahali ambapo wakimbizi wanapatiwa fursa ya pili. Tunawaangusha wakimbizi kwa kutowapatia fursa ya kukuza stadi na maarifa wanayoyahitaji kuwekeza katika mstakabali wao.”
Melissa Fleming anaongeza, “Vikwazo kwa elimu kwa wakimbizi vinazidi kuongezeka wanavyozidi kukua. Kwa hivyo hili linatengeneza mzunguko usiokuwa na mwisho. Usipokuwa na watoto katika sekondari, hawataweza kupata elimu ya juu hata kama ingekuwepo.”
Kupungua kwa kasi kwa kuwaandikisha wakimbizi kati ya shule za msingi na sekondari, ni matokeo ya moja kwa moja ya upungufu wa ufadhili kwa elimu ya wakimbizi, imeeleza ripoti ya UNHCR.
Matokeo yake, shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi limetoa wito kwa serikali, sekta binafsi, mashirika ya elimu na wachangiaji kuwasilisha michango yao ya kifedha kwa mkakati mpya unaolenga kusongesha elimu ya sekondari kwa wakimbizi.