Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni wakati wa msichana- Ripoti

Watoto wa kike wanapokuwa ukimbizini wanakuwa na fursa finyu zaidi ya kupata elimu
Margarida Loureiro/Archive
Watoto wa kike wanapokuwa ukimbizini wanakuwa na fursa finyu zaidi ya kupata elimu

Sasa ni wakati wa msichana- Ripoti

Utamaduni na Elimu

Wakati umefika wa kusema sasa basi na kupatia wasichana wakimbizi fursa ya kwenda shule hadi elimu ya juu ili waweze kujinasua kutoka lindi la umaskini na mateso, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR iliyotolewa hii leo ikipatiwa jina, #HerTurn.

Wasichana wakimbizi wana fursa finyu zaidi kuendelea na masomo ya sekondari kuliko wavulana wakimbizi, licha ya kwamba idadi yao ni kubwa.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ikisema sasa wakati umefika msichana kupatiwa kipaumbele.

Ikipatiwa jina wakati wake au “Her Turn”, ripoti hiyo inasema tayari mila zinazuia mtoto wa kike kwenda shule, sasa ukimbizi unazidi kufifisha fursa yake zaidi ya kuendelea hadi elimu ya sekondari.

“Milango ya elimu ya juu inafungwa kutokana na kuishi ukimbizini hivyo idadi ya wasichana wakimbizi kwenye elimu ya juu inakuwa ndogo,” imesema ripoti hiyo.

Akizungumzia ripoti hiyo, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema takwimu hizo ni kiashiria cha kutaka watu kuamka na kupaza sauti kwa ajili ya wasichana wakimbizi.

Msichana mkimbizi akifanya mtihani shule ya msingi Moghadishu kwenye kambi ya Kakuma nchini Kenya
UNHCR/S.Otieno
Msichana mkimbizi akifanya mtihani shule ya msingi Moghadishu kwenye kambi ya Kakuma nchini Kenya

Ametilia msisitizo hatua za kuchukua ikiwemo kutunga sera zinazotekelezeka akisema kuwa, “kusaka majibu ya kukabili changamoto hizi kwa wasichana wakimbizi pindi wanapohaha ili waende shule kunahitaji hatua mtambuka kuanzia wizara za elimu, vyuo vya mafunzo ya walimu, jamii hadi madarasani.”

Akiangazia fursa za ajira kwa wakimbizi, Kamishna Grandi amesema iwapo wakimbizi wataruhusiwa kufanya kazi, wataweza nao kuruhusu watoto wao waende shule bila kujali jinsia zao.

Ripoti inasema elimu kwa wakimbizi wasichana ni mbinu ya kujilinda dhidi ya madhila mbalimbali ikiwemo magonjwa, ukatili, unyanyasaji n ahata ndoa na mimba zisizohitajika.

Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 61 tu ya watoto wakimbizi ndio wanapata elimu ikilinganishwa na asilimia 91 ya watoto wasio wakimbizi.