UNHCR yataka Ulaya ichukue hatua kulinda watoto wakimbizi

14 Oktoba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifala kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetaka serikali za Ulaya zichukue hatua zaidi kulinda watoto wakimbizi na wahamiaji ambao wameendelea kukumbwa na machungu kando ya machungu waliyokumbana naoy wakati wa safari hatarishi kuingia barani humo.

UNHCR imesema hayo katika ripoti yake iliyochapishwa leo ikiangazia safari hatarishi kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu wa 2019, ikionesha kuwa watoto hao wamekumbwa na madhila kama malazi yasiyo salama, kusajiliwa kama watu wazima na kukosa huduma sahihi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo katika kipindi hicho kinachoangaziwa, takribani watu 80,800 waliwasili Ulaya kupitia bahari ya Mediteranea ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na watu 102,700 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Miongoni mwa waliowasili, zaidi ya robo ni watoto ambao wengi wao walisafiri bila wazazi.

“Watoto hawa wanaweza kuwa wamekimbia mapigaon, wakuwa mbali na nyumbani kwao kwa miezi au hata miaka wakikumbwa na madhila wakati wa safari, lakini machungu hayo hayokomei mpakani,” amesema Pascale Moreau, mkurugenzi wa UNHCR ofisi ya Ulaya.

Amefafanua kuwa katika maeneo mengi ya Ulaya, watoto wasioambatana na wazazi wanalundikwa kwenye vituo vikubwa bila mara nyingi bila ungalizi wowote, wakiwa hatarini kukumbwa na ukatili na hata kuwa na uwezekano wa watoto hao kutoweka.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ugiriki imepokea idadi kubwa ya watu hao walioingia Ulaya mwaka huu, zaidi ya Hispani, Malta, Cyprus na Italia.

Idadi kubwa ya watoto wameingia Ugiriki na wanatoka Afghanistan na Syria na mataifa mengine yaliyogubikwa na mizozo.

“Mazingira katika vituo vya mapokezi vilivyojaa pomoni kwenye visiwa vya Aegean nchini Ugiriki yanatia hofu kubwa. Mamlaka za Ugiriki zimetangaza hatua za kupungua mlundikano na kuna mwelekeo chanya ikiwemo watoto kupata walezi kwenye jamii,” imesema ripoti hiyo.

Hata hivyo ripoti imeongeza kuwa hadi mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba, idadi kubwa ya watoto wasio na walezi huko Ugiriki bado wana malazi yasiyo na uhakika na yasiyofaa.

Kwa mantiki hiyo, UNHCR imesema kwa kuzingatria hatari wanazokabiliwa nazo, “tunasihi nchi za Ulaya zifungue maeneo zaidi ya kuwahamishia watoto hao kama kitendo cha kuonesha mshikamano na kuongeza kasi ya kuhamisha watoto hao ili waungane na familia zao.”

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter