Sasa mkirudi nyumbani, wale watakaokuja huku muwaeleze waendelee kutusaidia- Mnufaika wa mafunzo DRC

29 Agosti 2019

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mafunzo ya ufundi cherehani yaliyotolewa na walinda amani wanawake kutoka Tanzania kwa wanawake wakazi wa mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini yameanza kuleta matumaini na kudhihirisha jukumu la ulinzi wa amani na uwezeshaji wa jamii nchini humo.

Ni katika wilaya ya Butsili, mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini ambako walinda amani kutoka Tanzania wanaoudumu kwenye kikundi cha  6 cha kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO wamekuwa wakitoa mafunzo ya upanzi bora wa mboga na ushoni.

Lengo ni kuimarisha ulinzi wa raia na wakati huo huo kuwawezesha kupata kipato na sasa mkuu wa kikundi cha wanawake wa Tanzania kwenye FIB,  Mercy Isaka wakiwa na wenzake wametembelea kujiona hali ikoje baada ya mafunzo.

Miongoni mwa wanufaika ni Marie Tekahindo ambaye alipoulizwa manufaa amesema, "watanzania walituita hapa wakatafuta wanawake tulikuwa watano tukaenda huku wakatufundisha kupanda mboga mboga kwamba kila mtu kwa kuwa tupo kwenye vita basi tunaweza kupanda mboga karibu na nyumbani. Unaweka udongo kwenye mfuko unachukua mbegu ya mboga unapanda na wakasema unaotenda pembeni ya nyumba.  Ndio wakatufundisha hiyo. Na cherehani wakatuambia kwamba hiyo haitoshi tuwapatie wengine mafunzo na tuwapatie vyerehani tuwafundishe kushona kwamba kule watakuwa wanaopanda mboga sasa wanapata na cherehani wanafungua mahala pa kushona nguo barabarani na hivyo  wanapata fedha kidogo wanasaidia watoto."

Pamoja na kupafa fedha za kusaidia watoto, Marie ameongeza kuwa,  “nimefaidika kwamba napata wateja napata mmoja mmoja. Hata mimi sasa nashona  nguo zangu badala ya kupeleka kwa fundi. Hata watoto wangu sasa nawanunulia kitengo na nawashonea nguo zao. Hiyo ndio mimi nashukuru na nyinyi msichoke kututakia mema hata kule nyumbani mtarudi salama na wale watakuja waendelee na sisi vizuri .”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter