Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa MONUSCO kutoka nchini Tanzania na Nepal watunukiwa Nishani

Kikundi Cha Bendera cha Pamoja cha Walinda Amani wa Tanzani na Nepali wakitoa Salamu kwa Mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani DRC, MONUSCO.
MONUSCO
Kikundi Cha Bendera cha Pamoja cha Walinda Amani wa Tanzani na Nepali wakitoa Salamu kwa Mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani DRC, MONUSCO.

Walinda amani wa MONUSCO kutoka nchini Tanzania na Nepal watunukiwa Nishani

Amani na Usalama

Vikosi vya Walinda Amani kutoka Tanzania Kwa kushirikiana Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa kutoka nchini Nepali wanaohudumu nchini Jamhuri ya Kidemkorasia ya Kongo – DRC wamefanya gwaride la pamoja na kutunikiwa Nishani za Umoja wa Mataifa na Mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani DRC, MONUSCO Luteni Jenerali Otavio Miranda Filho ikiwa ni kuthamini mchango wao wa kuhakikisha Amani ya Kudumu na Usalama vinapatikana nchini DRC.

Luteni Jenerali Filho ameeleza kufurahishwa na kuwashukuru walinda amani hao wa Tanzania na Nepali kwa Kazi nzuri katika kuhakikisha amani Mashariki ya Kongo inapatikana. “Nina furaha kubwa kwa hii nafasi ya kuwa hapa leo pamoja na vikosi vya Tanzania na Nepali ili kutambua kama Force Commander utekelezaji na mafanikio makubwa ya vikosi hivi. Vimefanya kazi nzuri sana na niko hapa kutambua hilo na kusema asante.”

Sherehe hizo za Kutunuku Medali za Umoja wa Mataifa zilizofanyika Mjini Beni Mavivi nchini DRC zilihudhuriwa na Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Wananchi la Tanzania, Meja Jenerali Marco Gaguti ambaye alimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.

Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) Meja Jenerali Marco Gaguti akimkabidhi zawadi Mwakilishi wa  Walinda Amani wa Jeshi la Nepal wanaohudumu chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO.
MONUSCO
Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) Meja Jenerali Marco Gaguti akimkabidhi zawadi Mwakilishi wa Walinda Amani wa Jeshi la Nepal wanaohudumu chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO.

Alitoa salamu za pongezi za Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, JWTZ Jenerali Jacob Mkunda, kwa maafisa na askari waliotunukiwa Medali na kusisitiza kuwa siku hii ni siku muhimu sana Kwa JWTZ, na ni siku ya Heshima kubwa katika  kutambua mchango wa Tanzania katika kuleta amani ya kudumu Nchini ya DRC.

Naye Kamanda Kikosi Cha 10 cha Tanzania (TANZBATT -10) Luteni Kanali John Kalabaka amefurahishwa kwa walinda amani kutoka Tanzania kutunukiwa Nishani ya Ulinzi wa Amani huko  DRC na kusema hiyo ni ishara ya kukubalika na Umoja wa Mataifa kwa kazi kubwa inayofanywa na na Walinda Amani kutoka Tanzania 

Kwa upande wake Meja Neema Alfred Neligwa  ambaye ni Matroni wa kikundi Cha Walinda Amani kutoka Tanzania nchini  DRC na Afisa mwanamke amesema wanawake wana Uwezo wa kufanya kazi za Ulinzi wa Amani na pia ni heshima kubwa kwao kutunukiwa Nishani za Umoja wa Mataifa.

Kwa mara ya Kwanza Nishani za Umoja wa Mataifa zilianza kutolewa mnamo mwaka 1950 hadi mwaka 1953 wakati wa Vita vya Korea 

Baadae, Mwaka 1955 Nishani nyingi za Umoja wa Mataifa zilianza kutolewa kwa watu wasio wanajeshi pia na Wanajeshi walioshiriki  opareshini mbali mbali duniani za kijeshi ama kipolisi katika matukio mbali mbali katika kuthamini mchango wao wa Ulinzi wa Amani Ulimwenguni.