Skip to main content

Mabadiliko  ya tabianchi hebu tusikilize sauti za vijana- Guterres

Vijana waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn Ujerumani wakiwa wamebeba kitambaa kilichoandikwa iokoe dunia. Mkutano huo ulihusu mabadiliko ya tabia nchini.
Photo/UNFCCC
Vijana waliohudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini Bonn Ujerumani wakiwa wamebeba kitambaa kilichoandikwa iokoe dunia. Mkutano huo ulihusu mabadiliko ya tabia nchini.

Mabadiliko  ya tabianchi hebu tusikilize sauti za vijana- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema anatambua shaka na shuku walizo nazo vijana kuhusu mustakabali wa mazingira lakini bado ana matumaini kwa siku za usoni.

Bwana Guterres amesema hayo leo katika ujumbe wake wa moja kwa moja kwa vijana na watoto walioandamana maeneo mbalimbali duniani hii leo wakitaka  hatua za dhati dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Ujumbe huo umechapishwa kwenye gazeti la The Guardian ambapo Katibu Mkuu amesema anaelewa wasiwasi wao kutokana na hatua walizochukua lakini ameongeza kuwa binadamu ana uwezo wa kufikia mafanikio makubwa, “sauti zetu zimenipa matumaini.

Kizazi changu kimeshindwa kuchukua hatua sahihi kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Hali  hii inatambuliwa vyema na vijana na ndio maana wana  hasira.

Hata hivyo Bwana Guterres amesema anaona dhamira na uanaharakati kutoka kwa vijana ambao wamechoshwa na kasi ya jamii ya kimataifa ya kushughulikia  ongezeko la joto duniani na amesema hiyo ndio inampatia matumaini ya kwamba kwa pamoja watashinda.

Amewaambia vijana hao kuwa kwa msaada wao na shukrani kwa jitihada zao wanaweza kushinda tishio hilo na kujenga dunia ambayo ni salama, safi, ya kijani kwa kila mkazi.

Akigeukia viongozi wa dunia, Guterres amesema “hawa wanafunzi wametambua kitu ambacho kinawapita idadi kubwa ya viongozi wao. Tupo kwenye mbio za maisha na tunashindwa. Fursa inayoyoma na hatuna tena muda wa kupoteza na tabianchi inayocheleweshwa ni sawa na tabianchi inayopotezwa.”

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, kiwango cha hewa chafuzi kinafikia rekodi ya juu zaidi na kinaendelea kuongezeka akisema kuwa kiwango cha hewa ya ukaa hivi sasa angani ni cha juu kuwahi kufikiwa katika miaka milioni 3 iliyopita.

Tweet URL

“Miaka minne iliyopita, imekuwa ni miaka yenye joto zaidi na viwango vya joto kwenye msimu wa baridi kali huko ncha ya kaskazini mwa dunia vimeongezeka kwa nyuzi joto 3 kwenye kipimo cha selsiyasi tangu mwaka 1990. Viwango vya maji ya bahari vinaongezeka, matumbawe yanaharibika na kuna ongezeko la tishio la afya kwa binadamu duniani kama ilivyowekwa bayana na ripoti ya hali ya mazingira duniani iliyochapishwa wiki iliyopita,” amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha kuwa mkataba wa kihistoria wa Paris kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015 uliotiwa saini nan chi 190 hautakuwa na maana iwapo hatua sahihi hazitachukuliwa.

Katibu amesema “ndio maana baadaye mwaka huu nitawaita hapa viongozi wa dunia. Natoa wito kwa viongozi wote waje New  York, mwezi Septemba wakiwa na mipango thabiti na halisi ili kushamirisha michango yao ya kitaifa ya kupunguza hewa chafuzi mwaka 2020 sambamba na mpango wa kupunguza kwa asilimia 45 hewa chafunzi ndani ya muongo mmoja ujao na kutokomeza kabisa mwaka 2050.”

Amesema kuwa kwa uchambuzi wa sasa, iwapo hatua sahihi zitachukuliwa, “tunaweza kupunguza hewa chafuzi ya ukaa ndani ya miaka 12 na kupunguza kiwango cha joto kwa nyuzi joto 1.5 lakini iwapo tutaendelea kwa mwelekeo wa sasa madhara yake hatuwezi kukadiria.”