Maelfu ya wakimbizi wa wanarejea nyumbani DRC wakitokea Angola-UNHCR

23 Agosti 2019

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Andrej Mahecic, hii leo mjini Geneva Uswisi amesema inakadiriwa kuwa wakimbizi 8,500 kwa hiyari yao wameondoka katika makazi ya wakimbizi ya Lóvua katika jimbo la Lunda Norte nchini Angola tangu tarehe 18 mwezi huu wa Agosti kwa lengo la kurejea nyumbani Jamhuri ya kidemkrasia ya DRC.

“Hii inaonekana kuwa mwitiko kwa ripoti za kuimarika kwa usalama katika baadhi ya maeneo wanakotoka na pia hamu ya kutaka kurejea nyumbani katika nyakati hizi za kuanza kwa mwaka wa masomo.” Amesema Andres Mahecic.

Bwana Mahecic ameeleza kuwa maelfu ya wakimbizi tayari wa,mevuka mpaka kuingia DRC na wengine wengi wanaelekea kwenye mpaka wa jimbo la Kasai.

Jimbo la Kasai linarejea katika hali yake baada ya mapigano kati ya makundi yenye silaha na vikosi vya serikali ya DRC mnamo mwaka 2017, mapigano ambayo yaliwatawanya watu milioni 1.4 kutoka katika makazi yao. Takribani wakimbizi 37,000 walivuka mpaka.

“Kurejea kwa hiyari kwa wakati huu kaskazini mashariki mwa Angola kunahusishwa na uchaguzi wa wa urais na pia kufuatia mazungumzo ya hivi karibuni kati ya viongozi wa DRC na wakimbizi ambapo wakimbizi walielezwa kuhusu kuimarika kwa hali ya usalama katika jimbo la Kasai.” Msemaji huyo wa UNHCR ameeleza.

Hadi kufikia sasa, kambi ya wakimbizi ya Lóvua, imekuwa ikiwahifadhi zaidi ya wakimbizi 20,000. Serikali ya Angola imewapa usafiri baadhi ya wakimbizi walioamua kurejea makwao.

UNHCR na wadau pamoja na seriali zote mbili wamejizatiti kuanzia nchini Angola, njiani, mipakani n ahata ndani ya DRC ili kuhakikisha wanafanya kila namna kuwapa usaidizi wakimbizi wanaorejea.  

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter