Maelfu ya wakongo kurejea nyumbani kutoka Angola

8 Oktoba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasaidia kuwarejesha nyumbani maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC waliokuwa wamesaka hifadhi Angola.

Msemaji wa UNHCR huko mjini Geneva, Uswisi, Charlie Yaxley amesema wakimbizi hao wamerejea eneo la Kasai ambako mapigano baina ya vikundi vilivyojihami yamepungua na hali ya usalama imeimarika.

“Kundi la kwanza la mamia ya watu hao litarejea nyumbani kupitia mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari, mpango ambao utaanza wiki hii kufuatia kutiwa saini tarehe 23 mwezi Agosti mwaka huu mkataba wa utatu baina ya serikali za Angola, DRC na UNHCR,” amesema Bwana Yaxley.

Amesema mpango  huo utahusisha jumla ya wakimbizi 4,000 watakaorejea nyumbani katika wiki zijazo na kwamba, “UNHCR inawapatia usafiri, msaada wa fedha pia kwa ajili ya kuwawezesha kujumuika kwenye jamii.”

Waliorejea awali tayari wanapatiwa msaada

Wakati huo huo, Bwana Yaxley amesema tangu tarehe 18 mwezi Agosti mwaka huu, wakimbizi 12,000 wa DRC wakiwemo watoto 7,000 wamerejea  nyumbani kutoka makazi ya muda ya Lovua kwenye jimbo la Lunda kaskazini nchini Angola.

“UNHCR inashukuru mamlaka za Angola kwa kusaidia kurejea haraka nyumbani kwa wakimbizi hao kwa kuwapatia usafiri wa lori hadi DRC,” amesema msemaji huyo wa UNHCR.

Taswira ya vizazi vitatu vilivyoathirika na machafuko Ndaya Monique wa umri wa miaka 60, na mwanae Mujinga Chantal na mjukuu wake Karumbu Léonard, 10 katika mkoa wa Kasai-Oreintal, DRC
UNICEF/Tremeau
Taswira ya vizazi vitatu vilivyoathirika na machafuko Ndaya Monique wa umri wa miaka 60, na mwanae Mujinga Chantal na mjukuu wake Karumbu Léonard, 10 katika mkoa wa Kasai-Oreintal, DRC

Yaelezwa kuwa idadi kubwa ya wanaorejea nyumbani wanakabiliwa na hali ngumu na mazingira magumu kwa hiyo UNHCR inawapatia kiasi cha fedha sambamba na misaada ya kibinadamu inayotolewa kwa pamoja na mashirika ya kiraia, mamlaka za majimbo  na wadau kwenye mpaka wa Kalamba Mbuji ambako UNHCR imeweka kituo cha muda.

UNHCR inasema misaada ya aina  hiyo pia wanapatiwa wale waliokwishawasili Kananga ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kasai.

“Ijapokuwa mapigano baina ya vikundi vilivyojihami yamepungua, baadhi ya wakimbizi hawana uhakika na jinsi watakuta  nyumba zao. Baadhi hawako tayari kurejea nyumbani kwao na hivyo wanasaka maeneo mapya, kwa kuwa wana hofu ya kwamba mapigano ya kikabila yataanza upya,” amesema Bwana Yaxley.

Miundombinu imesambaratishwa

UNHCR inasema kwenye eneo hilo la Kananga, miundombinu ya kijamii kama vile shule, vituo vya vya, imeharibishwa wakati wa mapigano hayo na bado haijakarabatiwa huku huduma za sasa bado hazikidhi mahitaji ya wakimbizi.

Kwa mantiki hiyo, UNHCR inaendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya DRC za kurejesha huduma za msingi na kuendeleza utangamano wa kijamii.

Tayari UNHCR na wadau wake War Child UK, wanaendesha tathmini kwenye maeneo ya Kananga na viunga yake ili kubaini hofu za kiusalama na kiulinzi na kuhakikisha hatua sahihi zinachukuliwa.

Hata hivyo ukata ni tatizo na hivyo  “msaada mkubwa wa fedha unahitajika kutoka jamii ya kimataifa ili mashirika ya kibinadamu na serikali ya DRC waweze kuweka mazingira endelevu kwa wakimbizi kurejea nyumbani,” amesema Bwaan Yaxley.

UNHCR inasema kuwa viwango vya sasa vya fedha za usaidizi viko chini ambapo kwa mwaka huu wa 2019 shirika hilo limepokea asilimia 57 tu ya dola milioni 150 zinazohitajika kusaidia waathirika wa janga la DRC.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter