Tusaidie manusura na waathirika wa ugaidi angalau kupunguza makovu yao- Guterres

21 Agosti 2019

Leo ni siku ya kimataifa ya kumbukizi na kutambua waathirika na manusura wa vitendo vya ugaidi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza kwenye tukio maalum lililofanyika katika makao makuu ya chombo hicho jijini New York, Marekani akisema kuwa ugaidi na aina zake zote umesalia changamoto kubwa.

Akihutubia tukio hilo lililohudhuriwa pia na waathirika wawili wa matukio ya ugaidi ya Kenya na Marekani pamoja na manusura mmoja wa tukio la ugaidi nchini Uingereza, Bwana Guterres amesema ugaidi umebakisha makovu ya kudumu kwa manusura na familia zao akiongeza kuwa ingawa muda unakwenda bado makovu hayo katu hayaishi 

Bila kujali tukio ni la lini, tusaidie waathirika na manusura

Hata hivyo amesema siku ya leo, ambayo ni mara ya pili kuadhimishwa tangu kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa miaka miwili iliyopita, “inatukumbusha kuwa bila kujali ni muda gani shambulio lilitokea, waathirika na manusura wanaendelea kuhaha na kilichowafika. Waathirika na manusura duniani kote wanahitaji fursa ya kupona majeraha kupitia haki na usaidizi.”

Katibu Mkuu amesema kuwa maelfu wanaonesha mnepo wa hali ya juu, ujasiri na nia ya hali ya juu, “wameunda ushirika wa kimataifa, wanashughulikia na kukabilina na fikra potofu zinazoenezwa na magaidi na wanapaza sauti zao dhidi ya vitisho vya ugaidi na ukosefu wa haki.”

Ni kwa mantiki hiyo Bwana Guterres amesema kuwa, “tunahitaji kuwapatia msaada wa muda mrefu, usaidizi mtambuka kwa waathirika na manusura wa ugaidi ikiwemo kupitai ubia na serikali, mashirika ya kiraia ili waweze kupona na kujenga upya maisha yao na wasaidie wengine.”

Amekumbusha kuwa Umoja wa Mataifa kwa kupitia kusikiliza na kusaidia manusura na waathirika wa ugaidi, umesaidia kuunganisha jamii dhidi ya ugaidi.

Bwana Guterres ametaja ofisi  ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi, UNOCT kama moja ya mbinu ya kutekeleza ahadi zake dhidi ya ugaidi akipongeza hatua za hivi karibuni za Baraza Kuu ya kupitisha azimio kuhusu waathirika pamoja na kuanzishwa kwa kikundi cha marafiki wa waathirika na manusura wa ugaidi.

Halikadhalika ametaja mkutano wa kimataifa wa waathirika wa ugaidi utakaofanyika mwakani akisema utasaidia kukidhi mahitaji ya makundi hayo.
 
Bwana Guterres amesihi wakazi wa dunia kutumia siku ya leo kutathmini maisha ya wale ambao maisha yao yamebadilishwa kutokana na vitengo vya ugaidi na kuwaonesha kuwa hawako peke  yao wanapopaza sauti za kutaka haki na kusaidiwa kupona makovu.

Muathirika wa ugaidi kutoka Kenya ataja kinachomwezesha kusonga mbele

Miongoni mwa waathirika wa ugaidi ni Sarah Tikolo kutoka Kenya ambaye mumewe aliuawa wakati wa shambulio la kigaidi la tarehe 7 mwezi Agosti mwaka 1998 kwenye ubalozi wa Marekani nchini Kenya.

Akihutubia hafla hiyo, Sarah amesema kuwa, “tukio lile lilibadili kabisa maisha yangu kwa sababu “niliachwa mjane nikiwa na umri wa miaka 21 na mtoto mwenye umri wa miezi minne.”

Hata hivyo Sarah anashukuru kuwa kupitia familia yake, ndugu jamaa na marafiki ameweza kuwa na mnepo kwenye maisha yake na alipata kazi katika ubalozi wa Marekani jijini Nairobi ambako sasa anafanya kazi kuweza kukimu maisha yake.

“Nimeweza kumudu maisha kutokana na uwepo wa ndugu jamaa na pia kupitia kazi hii naweza kusomesha mwanangu wa kiume ambaye sasa yupo Chuo Kikuu,” amesema Sarah ambaye ameusihi Umoja wa Mataifa usake zaidi mbinu za kusaidia manusura na waathirika wa ugaidi ambao amesema wengi wao sauti zao hazisikiki au hazisikilizwi.

TAGS: Ugaidi, Manusura wa Ugaidi, UNOCT, Sarah Kikolo, Kenya, Antonio Guterres 
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud