UN  yazindua mpango wa kudhibiti ugaidi kwa kufuatilia taarifa za wasafiri

7 Mei 2019

Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake ya kukabiliana na ugaidi, UNOCT leo umezindua mpango wa kudhibiti ugaidi kwa kufuatilia wasafiri.

Uzinduzi huo umefanyika wakati wa kikao cha ngazi ya juu kilichofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema mpango huo unaohusisha kuanzishwa kwa vitengo vya safari katika nchi husika, umekuja wakati muafaka kwa kuwa zama za sasa kune mienendo mingi inayohusisha wapiganaji wa kigeni na magaidi kusafiri kutoka kona moja hadi nyingine ya dunia.

“Miaka miwili tu iliyopita, tulikadiria kuwa zaidi ya wapiganaji magaidi wa kigeni 40,000, kutoka zaidi ya nchi 110 walisafiri kujiunga na makundi ya kigaidi nchini Syria na Iran. Na kufuatia kitendo cha magaidi wa ISIL kufurushwa kwenye maeneo yao, magaidi wengi wanajaribu kurejea nyumbani au wanasaka maeneo salama au kwingineko kwenye mapigano,” amesema Guterres.

Amesema wengi wao wana mafunzo ya hali ya juu wanaweza kufanya mashambulizi na wengine wana matumaini ya kusaka wafuasi wapya, kwa hiyo, “kuwabaini na kusambaratisha magaidi hawa na wahalifu wengine hatari kabla hawajafanya shambulio ni kipaumbele cha jamii ya kimataifa.”

FAIDA ZA MPANGO HUO

Katibu Mkuu amesema Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na azimio namba 2396 la Baraza la Usalama yamesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana taarifa katiika kuboresha uwezo wa kubaini na kuzuia safari za magaidi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, mpango huo “utasaidia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kukusanya, kuchakata na kubadilishana taarifa za safari na mamlaka nyingine bobezi za kitaifana kimataifa huku wakiheshimu faragha na masuala mengine.”

JE MPANGO UTAFANYA VIPI KAZI?

Akifafanua kuhusu mpango huo, Jelle Postma, ambaye ni mkuu wa kitengo cha safari na usalama wa anga katika ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na  ugaidi, amesema kile ambacho mataifa yatatakiwa kufanya.

Amesema  “ni kuanzisha kile ambacho kinaitwa kitengo cha taarifa za wasafiri ambacho kinapokea taarifa za safari na kulinganisha na kanzi data za watu tunaowafahamu  kama ni magaidi au mitandao hatari na kulinganisha na vigezo hatarishi kwa lengo la kutambua mitandao mipya ambayo inawezakuwa  hatari. Hii inatakiwa kuanzishwa kwa sheria kuhusu kulinda taarifa na masuala ya haki za  binadamu. Huu ni mfumo mzuri sana lakini pia kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa kuzingatia utunzaji wa takwimu na haki za binadamu.”

Bwana Postma amesema Umoja wa Mataifa utasaidia serikali kufuatilia raia wake pindi wanaporejea lakini pia wengine walio kwenye mpito kuelekea maeneo mengine kwa sababu “ magaidi wengine hawarejea nyumbani  bali wanapanga safari kwenda maeneo mengine na kupanga mashambulizi mapya.”

Amesema mpango  huu utasaidia kufuatilia magaidi wanaojulikana na pia kufichua wengine ambao hawafahamiki ambao wanasafiri kwa makundi.

MAJUKUMU YA UNOCT

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ugaidi ilianzishwa mwaka 2017 kwa ajili ya pamoja na mambo mengine kusaidia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na ugaidi. Halikadhalika kupanua wigo wa mtandao wa kubadilisha taarifa ili kubaini, kutambua, kusambaratisha na kushtaki magaidi.

Ofisi hiyo pia ina jukumu la kuhakikisha nchi wanachama ambazo zinaathirika zaidi na ugaidi zina uwezo wa kukabiliana na vitisho hivyo ambavyo hubadilika mara kwa mara.

Mataifa ambayo  hivi karibuni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yamekumbwa na mashambulio ya kigaidi ni Kenya, New Zealand nan a Sri Lankda akisema ni matukio ambayo  yanadhihirisha umuhimu wa ushirikiano na wadau mbalimbali, ikiwemo Umoja wa Mataifa na wengineo.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud