Mgawanyiko Mashariki ya Kati ni mkubwa lakini kuna fursa ya kutatua- UN

20 Agosti 2019

Eneo la Mashariki ya Kati lina mgawanyiko mkubwa lakini ndaniya changamoto hizo kuna fursa hatimaye mustakabali wenye nuru kwa wakazi wa eneo hilo.

Ni kauli ya aliyotoa leo Jumanne msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Maria Luiza Viotti wakati wa mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama kuhusu changamoto zinazokabili Mashariki ya Kati uliolenga kutambua changamoto hizo na hatua za kuchukua.

“Mashariki ya Kati imesalia kuwa eneo lenye matatizo magumu, yenye kuzingirwa na mizozo na mapigano, mivutano ya kijiografia iko katika ngazi ya kikanda, masuala ya utawala pamoja na kutumbukiza mataifa mengi ya ukanda huo kwenye mkwamo wa kiuchumi na kijamii,” amesema Bi. Viotti.

Ingawa hivyo amesema mwaka uliopita akihutubia Baraza hili, “Katibu Mkuu Antonio Guterres alisema kuwa mifumo iliyokuwepo kushughulikia hatari na mwendelezo wa mizozo kwenye eneo hilo hivi sasa haipo tena,” amesema Bi. Viotti akiongeza kuwa “mawazo yetu ya pamoja ni kwamba ni lazima tupate njia kwa eneo hili lililo tajiri kwa rasilimali watu na maliasili ili kufikia uwezo wake na kunufaisha watu wote.”

Changamoto zilizopo ni lukuki

Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametanabaisha mivutano iliyopita Mashariki ya Kati ikiwemo matukio ya hivi karibuni kwenye mfereji wa Hormuz ambako mataifa yanavutana juu ya matumizi ya mfereji huo.

“Ni muhimu sana haki na wajibu vinavyohusiana na usafirishaji kwenye mfereji huo vikafanyika kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” amekumbusha Bi. Viotti.

Kuhusu Iran amesema kuna mvutano mkubwa juu ya mpango wa nyuklia wa Iran akisema kuwa, “mwendelezo wa kutokukubaliana kutazidi kuongeza mvutano kwenye eneo la ghuba.”

Kuhusu Syria amesema mapigano yanayozidi kushamiri kaskazini-magharibi mwa taifa hilo yanatilia shaka uwezekano wa Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Geir Pedersen kufufua mchakato wa kisiasa.

Akiangazia Yemen, amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kusambaza misaada ya kibinadamu inayohitajika zaidi nchini humo wakati Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa Yemen, Martin Griffiths akiendelea na jitihada za kutekeleza mkataba wa Hudaidah.

Familia ambazo zinakaa kambini karibu na mpaka na Uturukikufuatia uhasama unaoshuhusiwa jimbo la Idlib na Aleppo.(Juni 2019)
© UNICEF/UN0318979/Ashawi
Familia ambazo zinakaa kambini karibu na mpaka na Uturukikufuatia uhasama unaoshuhusiwa jimbo la Idlib na Aleppo.(Juni 2019)

Kwa upande wa mzozo kati ya Palestina na Israel, Bi. Viotti amesema bado unasalia kuwa ni mzozo wa muda mrefu zaidi katika ajenda ya amani na usalama ya Umoja wa Mataifa.

“Suluhu ya haki inayokubalika pande zote ni muhim ukwa mustakabali bora wa ukanda wote wa Mashariki ya Kati,” amesema Bi. Viotti.

Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu amegusia pia ugaidi akisema kuwa harakati zozote za kukabiliana na ugaidi lazima ziende sambamba na kuheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa.

Akitamatisha amesema orodha ya changamoto ni kubwa lakini zisiwavunje moyo na badala yake hatua muhimu hi kuzuia viashiria vya mizozo kwenye eneo hilo visilipuke.

“Kufungua njia za mawasiliano ni kipaumbele cha kwanza ikifuatiwa na kujengeana imani ili pande zote ziondoke kwenye mvutano na ziingie kwenye mashauriano,” amesema Bi. Viotti akisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa kwa upande wake unakabiliana na changamoto hizo kwa njia mbalimbali ikiwemo diplomasia ya kuzuia mizozo, kusambaza misaada ya kibinadamu, kuunga mkono mikakati ya maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amekumbusha kuwa jukumu la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa Katiba, la kusongesha amani ya kimataifa na usalama linasalia kuwa muhimu kuliko wakati wowote.

Sasa hatusikiliza maneno tunaangalia vitendo- Pompeo

Mkutano huo ulioandaliwa na Poland, ulihutubiwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Michael Pompeo ambaye amesema kuwa “serikali ya Marekani imeanzisha mwelekeo mpya wa kushughulikia eneo la Mashariki ya Kati.”

“Tunachofanya sasa tunashirikiana na wadau mbalimbali na hatutasilikiza maneno bali tunaangalia vitendo,” amesema Bwana Pompeo ambaye serikali yake na Poland mwezi Februari mwaka huu walianzisha mazungumzo kuhusu Mashariki ya Kati ukipatiwa jina mchakato wa Warsaw.

Amewaambia wajumbe kuwa hivi sasa kwenye mchakato huo wameunda vikundi kazi 7 vikiangazia usalama wa mtandao, haki za binadamu, usalama wa usafirishaji majini, wakimbizi, usalama wa nishati, uenezaji wa makombora na masuala ya kibinadamu.

“Hakuna taifa moja ambalo litatawala mjadala huu, mataifa yote yatasikilizwa na  sauti zote zitaheshimiwa,” amesema Bwana Pompeo.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter