Bila kuungana katu hatuwezi kupata amani ya kudumu- Guterres

16 Februari 2018

Hali ya usalama duniani inazidi kukumbwa na vitisho kila uchao, mizozo ikizidi kuimarika na wapiganaji wakihamahama ili kutekeleza vitendo vyao viovu. Kinachotakiwa sasa ni dunia kuungana kwani wahenga walisema "Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu."

Vitisho vya usalama vinavyokumba duniani hivi sasa vinahitaji ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kukabiliana navyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo leo huko Munich Ujerumani wakati akihutubia mkutano wa kimataifa kuhusu usalama duniani.

Amesema ingawa vitisho vya usalama vilikuwepo tangu zama za kale lakini hali imekuwa mbaya zaidi tangu kumalizika kwa vita baridi akitaja maeneo mawili yanayoleta shaka na shuku kubwa.

Mosi Bwana Guterres ametolea mfano kitisho kikubwa zaidi cha silaha za nyuklia wakati huu ambapo silaha za nyuklia zinaendelezwa sambamba na makombora ya masafa marefu yanayotengenezwa na Korea Kaskazini.

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Na hoja ya kutokomeza nyuklia, kwa mtazamo wangu inahitaji sote tushiriki kwa kina ili hatimaye wadau wawili muhimu kwenye mzozo huu ambao ni Marekani na Korea Kaskazini waweze kukaa pamoja na kuwa na mjadala wa dhati kwenye masuala haya. Naamini Marekani iko tayari kufanya  hivyo.”

Ametaja jambo la pili kuwa ni mzozo wa Mashariki ya Kati akisema awali ilikuwa ni kati ya nchi lakini sasa mizozo inazidi kushamiri na kuhusiana na kuleta changamoto katika utatuzi. Kwa mantiki hiyo amesema..

Moja ya mitaa huko Douma, eneo la Ghouta mashariki nchini Syria ambako mapigano yamesambaratisha maeneo ya makazi.
UNICEF/Amer Al Shami
Moja ya mitaa huko Douma, eneo la Ghouta mashariki nchini Syria ambako mapigano yamesambaratisha maeneo ya makazi.

 

 

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Hali katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati kwa mtazamo wangu ni kitisho tofauti kabisa ambacho kinahitaji kuhamasisha juhudi zetu zote ili tuweze kushughulikia.”

Katibu Mkuu amesema inaweza kuonekana kuwa ni jambo la hila kuwa kwa kiwango cha migongano hivi sasa ni vigumu sana watu kuungana lakiini anadhani ni hila kuamini kuwa katika mgawanyiko dunia inaweza kukabili changamoto za sasa hivyo amesema..

“Kwa  hiyo wito wangu mkuu hii leo ni tumaliza tofauti zetu, tumalize migongano yetu na tuelewe kuwa kukabili changamoto zote zinazomkabili binadamu hivi sasa bila shaka ni lazima tuwe kitu kimoja.”

Mkutano huo wa siku tatu ulioanza leo utamalizika jumapili na umeleta pamoja viongozi wa ngazi za juu ikiwemo marais na mawaziri.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter