Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa una wasiwasi na hali inavyoendelea Yemen

Mtoto akitembea kwenye magofu huko Craiter mjini Aden nchini Yemen. Eneo hili liliharabiwa kwa kiasi kikubwa na makombora yaliyoangushwa kutoka angani mwaka 2015 wakati vikosi vya washirika vilipokuwa vikifurumusha wahouthi.
OCHA/Giles Clarke
Mtoto akitembea kwenye magofu huko Craiter mjini Aden nchini Yemen. Eneo hili liliharabiwa kwa kiasi kikubwa na makombora yaliyoangushwa kutoka angani mwaka 2015 wakati vikosi vya washirika vilipokuwa vikifurumusha wahouthi.

Umoja wa Mataifa una wasiwasi na hali inavyoendelea Yemen

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo mjini New York, Marekani kujadili hali ya Yemen ambapo viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa wamelieleza baraza hilo kuhusu wasiwasi wao juu ya machafuko yanayozidi kuongezeka katika maeneo mengine ya Yemen na nje ya mji wa bandari wa Hudaidah ambako mkataba wa kusitisha mapigano unaendelea kutekelezwa.

Mark Lowcock ambaye ni Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, ameliambia Baraza la Usalama, “wakati usitishaji mapigano mjini Hudaidah unaendelea kuheshimiwa, tumeshuhudia kuongezeka kwa vurugu katika maeneo mengine ya nchi kama kule Hajjah, kaskazini mwa Hodeida na kule Taëz”

Bwana Lowcock ameongeza kusema kuwa wakati jumuiya ya kimataifa inaendelea kuunga mkono makubaliano ya Stockholm, Sweden yaliyofikiwa mwezi Desemba 2018 yaliyoamua uwekaji silaha chini, ni muhimu kutofumbia mamcho kinachoendelea katika maeneo mengine ya nchi amvako vurugu zinaendelea.

Kuhusu hali ya kibinadamu, Bwan Lowcock ameonya kuwa kuna uwezekano wa mlipuko wa kipindupindu ambapo tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2019, takribani visa 200,000 vya kipindupindu vimeripotiwa. Hiyo ni takribani mara tatu zaidi ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita yaani 2018. Takribani robo ya visa vyote ni watoto chini ya umri wa miaka mitano, amesema.

Aidha Lowcock amezisihi nchi zilizotoa ahadi ya kuchangia, kutekeleza ahadi zao mapema iwezekanavyo kwani mashirika ya Umoja wa Mataifa yataishiwa fedha. Mwezi Februari mwaka huu wachangiaji waliahidi dola bilioni 2.6 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu nchini Yemen lakini hadi sasa kiasi kilichopokelewa n idola milioni 267.

Baraza la Usalama likijadili Yemen na kwenye skrini ni Mark Lowcock, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA
UN /Loey Felipe
Baraza la Usalama likijadili Yemen na kwenye skrini ni Mark Lowcock, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA

Kwa upande wake Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Martin Griffiths amesema tangu kusitishwa kwa mapigano, vurugu katika mji wa Hudaidah zimepungua kwa kiasi kikubwa, na inaonekana ni kama wananchi wameanza kurejea makwao.

Kwa mujibu wake ni kuwa bado kuna mengi yanayotakiwa kufanywa ili kuitunza hali hiyo ya usitishwaji mapigano lakini angalau kuna maendeleo chanya ambayo yameonesha kinachoweza kufikiwa kupitia mazungumzo na kuvumiliana.

Amegusia pia mpango ambao umekubaliwa kati ya vikosi vinavyounga mkono serikali na waasi wa kihouthi ya kuondoa vikosi kutoka mstari wa mbele wa mapigano  kwenye mji wa Hudaidah na viunga vyake, ingawa amesema bado dalili za mapigano ziko kwenye maeneo mengine.

Kuhusu uchumi amesema bado hali ya uchumi ya Yemen bado inasalia kuwa katika hali tete, meli za biashara zinapata ugumu mkubwa kuifikia bandari ya Hodeida na bei ya mafuta imepanda sana.

Naye mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na migogoro ya silaha Bi Virginia Gamba amesema watoto nchini Yeman wanatakiwa kuwekwa katika msingi wa mchakato wa amani.