Warohingya wapatiwa vitambulisho; ni mara ya kwanza katika maisha yao

9 Agosti 2019

Kwa mara ya kwanza katika maisha yao, zaidi ya warohingya nusu milioni kutoka Myanmar walio ukimbizini nchini Bangladesh wamepatiwa vitambulisho.

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema waliopatiwa ni wale wenye umri wa miaka 12 na kuendelea na vitambulisho hivyo vitasaidia pamoja na mambo mengine kufahamu idadi na mahitaji yao.

“Hadi Jumatano ya wiki hii, zaidi ya warohingya 500,000 kutoka

Myanmar wamesajliwa katika operesheni ya pamoja iliyoendeshwa na mamlaka za Bangladesh na UNHCR,” amesema Andrej Mahecic alipozungumza na wanahabari hii leo mjini Geneva, Uswisi.

Amesema kwa idadi kubwa ya wakimbizi hao, ni mara ya kwanza kuwa na vitambulisho katika maisha yao. “Vitambulisho hivi vinavyotumia viungo kama vile macho na vidole ni kadi zisizoweza kughushiwa na zinatolewa kwa pamoja na Bangladesh na UNHCR kwa warohingya wenye umri wa zaidi ya miaka 12,” amesema Bwana Mahecic.

Msemaji huyo ameongeza kuwa kazi ya usajili inafanyika katika makazi yote ya wakimbizi huko Cox’s Bazar na “lengo ni kuhakikisha uhakika wa takwimu za wakimbizi hao walioko Bangladesh, na hivyo kupatia mamlaka za kitaifa na wadau wa kibinadmau uelewa mzuri zaidi wa idadi ya wakimbizi na mahitaji yao.”

Bwana Mahecic ameongeza kuwa, “takwimu sahihi zitasaidia mashirika kujipanga vizuri zaidi na kuweza kupeleka misaada inayohitajika zaidi kwa makundi kama vile wanawake na watoto na watu wenye ulemavu.”

Vitambulisho hivyo vipya vinaonesha kuwa Myanmar ni nchi  ya asili ya warohingya, kitu ambacho ni cha msingi zaidi katika kulinda  haki za kabila hilo za kurejea nchini mwao pindi na iwapo watataka kufanya hivyo.

Takribani wakimbizi 900,000 wa kabila la Rohingya wanaishi kwenye makazi yaliyojaa kupindukia huko Cox’s Bazar nchini Bangladesh ambapo zaidi ya 740,000 kati yao walikimbia Myanmar tangu mwezi Agosti mwaka 2017 kutokana na mateso.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter