Mradi wa ufumaji Cox’s Bazar kunusuru wanawake wakimbizi warohingya

16 Aprili 2019

Mradi mpya wa mafunzo unaotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa ajili ya kujenga uwezo wa kujitegemea kwa wanawake wakimbizi wa kabila la Rohingya na jamii zinazowahifadhi huko Cox’s Bazar nchini Bangladesh umeanza kuzaa matunda.

Ukitekelezwa kwa ushirikiano baina ya UNICEF na mashirika ya kiraia ikiwemo taasisi ya Ayesha Abeid, mradi huo ulioanza mwezi Februari unawapatia stadi kama vile ufumaji na uwekaji wa picha na maandishi kwenye vitambaa pamoja na ushoni ambapo tayari vituo 18 vidogo vinafunguliwa kwenye maeneo mengine ya Cox’s Bazar.

Liz Throssel ambaye ni msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi amewaambia waandishi wa habari kuwa,

(Sauti ya Liz Throssel)

 “Ndani ya mwaka mmoja ya mradi huu, lengo ni kufundisha wanawake 500, nusu yao wakiwa ni wakimbizi. Matarajio ni kwamba iwapo mradi huu  utakuwa wa mafanikio, unaweza kupanuliwa kufundisha mamia zaidi. Wakati wa mafunzo ya miezi sita wanawake wanapatiwa fedha kidogo.”

UNHCR ndio inafadhili mradi huu na ina imani kuwa baadaye unaweza kuleta faida.

Bidhaa tarajiwa kwenye mradi huu ni vitambaa vilivyofumwa na wakimbizi, mavazi ya watoto, wanawake na wanaume pamoja na vifaa vya matumizi ya ndani  ya nyumba na zitauzwa kwenye moja ya maduka mashuhuri nchini Bangladesh, Aarong.

Bi. Throssel amesema idadi kubwa ya wanawake wakimbizi wanaoshiriki mradi huo ni wajane au wanawake wasio na waume wakiwa na umri ya kati ya miaka 18 hadi 40 na hawana uzoefu wowote kwenye ushoni.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter