Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko yanayoendelea Rakhine na Chin yanatutia hofu-UNHCR

Mtoto akiwa katika makazi katika kambi ya Kyein Ni Pyin jimbo la Rakhine, Myanmar.
UNICEF/Ruslana Sirman
Mtoto akiwa katika makazi katika kambi ya Kyein Ni Pyin jimbo la Rakhine, Myanmar.

Machafuko yanayoendelea Rakhine na Chin yanatutia hofu-UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linafahamu kuhusu ripoti za kuongezeka kwa machafuko na kuzorota kwa hali ya usalama kusini mwa jimbo la Chin na Rakhine nchini Myanmar na ni suala linalowatia hofu kubwa.

Kwa mujibu wa shirika hilo hali hii imesababisha wakimbizi wa ndani na wakimbizi wapya kutoka Myanmar kusaka usalama kwenye jimbo la Bandarban mpakani mwa Bangladesh.

Akizunguza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic amesema hofu yao kubwa ni athari za hali ya kibinadamu na uwezekano wa ongezeko la wimbi la wakimbizi wa ndani na wakimbizi wapya na kwamba

(SAUTI YA MAHECIC)

”Kama sehemu ya juhudi za mashirika mbalimbali UNHCR iko tayari kusaidia masuala ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika nchini Myanmar. UNHCR pia imejitolea kuisaidia serikali ya Bangladesh kutathimini na kushughulikia mahitaji ya watu ambao wamewasili kusaka usalama wakikimbia machafuko Myanmar.”

Ameongeza kuwa wanaishukuru serikali ya Bangladesh kwa ukarimu wake na uongozi iliouonyesha kwa kupokea Zaidi ya wakimbizi 720,000 kutoka Myanmar tangu mwezi Agosti 2017.

UNHCR imetoa wito kwa uongozi wa Bangladesh kuendelea kuruhusu watu wanaokimbia machafuko nchini Myanmar kusaka usalama nchini Bangladesh.