Dunia isiwageuzie kisogo warohingya-Angelina Jolie

7 Februari 2019

Angelina Jolie, mjumbe maalumu wa shirika la la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wiki hii akitembelea Bangladesh amesema dunia haipaswi kuwageuzia kisogo wakimbizi wa Rohingya wanaokadiriwa kuwa milioni moja wakiwa wamekimbilia Bangladesh wakitokea Mynmar. Jolie ameomba wale wasio na makazi wasaidiwe hadi pale ambapo mamalaka za Mynmar zitaonesha nia thabiti inayohitajika kukomesha mzunguko wa mapigano uliodumu kwa miongo kadhaa.

Jana katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka, Angelina Jolie amefanya mkutano na waziri mkuu Sheikh Hasina na baadaye waziri wa mambo ya nje AK Abdul Momen ambapo ameeleza shukrani za dhati za UNHCR kwa wat una serikali ya Bangladesh kwa moyo wao wa kuwapokea zaidi ya wakimbizi 700,000 tangu agosti 2017. Aidha Jolie amerejelea juhudi za UNHCR za kusaidia warohingya kuishi maisha bora nchini Bangladesh na kutafuta suluhu ya kudumu. Ameeleza pia bila kupanua na kuimarisha fursa za elimu, kizazi kijacho cha warohingya kitakuwa hatarini.

Jumatatu Angelina Jolie alianza safari ya siku tatu katika kambi ya Chakmarkul na Kutupalong ambako amesikiliza shuhuda mbalimbali kutoka kwa wanawake wa Rohingya, Watoto na wanaume ambao wameishi maisha yao yote katika mateso na kukandamizwa. Pia ametembelea kituo kinachowapokea wakimbizi wapya wanaoingia na akajionea hospitali ambayo inatoa huduma za msingi zinazohitajika kuwasaidia wanawake na wasichana.

Ziara ya Angelina Jolie imekuja kabla ya ombi jipya la UNHCR ambalo litazinduliwa wiki ijayo ambapo shirika hilo linakusudia kuomba zaidi ya dola milioni 920 za kusaidia wakimbizi wa Rohingya pamoja na jamii zilizoathirika katika mwaka huu wa 2019.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter