Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vilabu vya Dimitra ni mkombozi kwa wakazi wa vijijini Afrika

Wanawake katika jimbo la Copperbelt nchini Zambia wanaofanya kazi katika mfumo wa kilimo bora wanaongeza uzalishaji wa mbogamboga wanaouza katika masoko ya wenyeji( kutoka maktaba 2015)
ILO/Marcel Crozet
Wanawake katika jimbo la Copperbelt nchini Zambia wanaofanya kazi katika mfumo wa kilimo bora wanaongeza uzalishaji wa mbogamboga wanaouza katika masoko ya wenyeji( kutoka maktaba 2015)

Vilabu vya Dimitra ni mkombozi kwa wakazi wa vijijini Afrika

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema vilabu vya Dimitra vimekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo vijijini na kubadili maisha ya takribani wakazi milioni 2 wa eneo hilo. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

FAO inasema katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kuna jumla ya vilabu 3,400 vya Dimitra, jina hilo likiwa asili yake ni Ugiriki likimaanisha mungu wa kilimo na ustawi.

Vilabu  hivyo ni vikundi vya hiari vya wanawake, wanaume, vijana ambao kwa pamoja hujadili matatizo yao na kusaka mbinu bora ya pamoja na endelevu ya kutatua kwa kutumia rasilimali walizo nazo,

Changamoto ni kama vile mabadiliko ya tabianchi, elimu, afya, miundombinu na lishe ambapo FAO inasema mambo makuu manne yamekuwa msingi wa vilabu vya Dimitra kwa miaka 10 sasa.

Mosi kukabiliana utapiamlo kwa kutokomeza mila potofu kwenye lishe, kusuluhishi mizozo ya muda mrefu ya kisiasa, kuhamasishana kulinda mazingira na kuunda vikundi vya kuweka na kukopa.

Suwebya Ide ni mnufaika kutoka Niger na baada ya kushiriki vilabu hata mavuno ya vitunguu shambani mwao yameshamiri akisema kwamba, “nina furaha sana, siwezi ficha furaha yanagu. Katu sikuwahi fikiria mabadiliko haya katika maisha yangu.”

Naye Francois Bassay mkaguzi wa kilimo kutoka jimbo la Tshopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni shuhuda wa  mafanikio ya vilabu vya Dimitra akieleza kuwa, “nimeshuhudia mabadiliko. Wali nilipotembelea vijiji nikiwa mkaguzi wa kilimo, watu walikuwa wanaomba mapanga, mbegu. Lakini sasa hawaniombi chochote, badala yake wanasema njoo ushuhudie kile tulichofanya”